HabariNews

Usalama imara; Tuktuk na Pikipiki zapigwa marufuku kuingia Mama Ngina Waterfront

Onyo limetolewa kwa watu wanaolenga kutekeleza uhalifu katika maeneo ya kujivinjari msimu huu wa sherehe.

Akizungumza na waaandishi wa habari katika Bustani la Mama Ngina hapa Mombasa Naibu Kamisha wa kaunti hiyo Ronald Muiwawi amesema wameweka mikakati kabambe kuimarisha usalama wa wanaozuru maeneo ya starehe na kuwachukulia hatua za kisheria watakaojaribu kukaidi suala hilo.

“Kitengo chetu cha usalama tukishirikiana na serikali ya kaunti ya Mombasa tumeweka mikakatin maalum kuhakikisha usalama wa kutosha.” Alisema.

Muiwawi aliwahimiza wakazi kushirikana na idara za usalama ili kufanikisha mchakato wa kudumisha halii ya utulivu na amani maeneo ya kujivinjari hususan msimu huu wa sherehe.

“Tunawaomba wakazi wa Mombasa watusaidie kwa kuwajibika pia hasa kwa wale vijana waendeshaji wa pikipiki tunajua kuna wale wanaootea msimu huu wa sherehe wanadhani ni msimu wao wa kuvuna; tunawaonya msimu huu hautakuwa wa kuvuna tuko macho, usalama tuliopangilia ni wa kutosha,” alisema Muiwawi.

Kwa upande wake Mratibu katika Bustani la Mama Ngina Waterfront, Bw. Ali Nuru aliwataka wanaozuru bustani hiyo pamoja na maeneo mengine ya starehe kaunti hii kutii kanuni na sheria za maeneo hayo ili kuepuka kujipata katika matatani wakikabiliwa na mkono wa sheria.

“Tunachoomba Wakenya wenzetu watakapokuja hapa waangalie na kufuata zile taratibu na kanuni za hapa, waangalie isije wakajipata kwenye mkono wa sheria,” alisema.

Aidha Bw. Nuru aliweka wazi kuwa wanaotumia usafiri wa bodaboda na tuktuk hawatoruhusiwa katika bustani hilo msimu huu wa sherehe kama njiamoja wapo ya kudhibiti visa vya uhalifu eneo hilo.

“Usalama wa kutosha hapa upo na watu watajivinjari bila bughdha yoyote , lakini kwa sababu za kiusalama Bw. Naibu kamishna ameeleza matatizo yanayokuja na uendeshaji wa pikipiki, kwa hivyo tumepiga marufuku pikipiki na tuktuk, zote kwa kipindi hiki hazitaruhusiwa hapa ili kuwa na shughuli bila taabu yoyote,” alisema.

Naye Mratibu wa Shirika la Msalaba Mwekundu kaunti ya Mombasa Aisha Hussein amesema watakuwa angae kukabiliana na majanga pindi yanapotokea ili kutoa usaidizi kwa muda ufaao.

BY BEBI SHEMAWIA