Hatimaye simba mla watu aliyemwua kijana mmoja mhudumu wa bodaboda kaunti ya Kwale wiki
moja iliyopita amekamatwa na kuuawa.
Simba huyo amelazimika kuuawa kwa mujibu wa kanuni na desturi ya shirika la wanyamapori nchini, KWS.
Akithibitisha taarifa hiyo wakati wa mahojiano na kituo kimoja cha habari hapa Pwani Naibu Msemaji wa
Serikali Mwanaisha Chidzuga amesema kuwa tayari simba huyo ameuawa na sasa wenyeji wapo huru
kuendeleza shughuli zao pasi na uoga.
Hata hivyo kiongozi huyo amewataka wenyeji hao kuchukua tahadhari kabla ya hatari na kuwa waangalifu
zaidi nyakati za usiku ili kuepukana uvamizi wa wanyamapori wengine hatari. “Yule simba mla watu ameweza
kukamatwa na kuuliwa, unajua katika desturi ya Wanyamapori KWS simba akiua watu lazima auawe, huwa
ashaonja damu so lazima auawe asiwe kwenye mbuga, ni salama zaidi. Tunawaambia wakazi watoe hofu lakini
tunawasihi waendelee kuwa waangalifu zaidi maana kuna ndovu na kuna nyoka, vyema wajihadhari, so if you
can waepuke kutumia barabara zile nyakati za usiku,” alisema.
Simba huyo mla watu alidaiwa kumshambulia na kumwua mhudumu mmoja wa bodaboda eneo la Marere katika
barabara ya Kwale-Kinango, ambapo mwili wa jamaa huyo ulipatikana kando ya pikipiki hiyo ukiwa umeliwa
sehemu za tumboni na chini.
BY DAVID OTIENO