Viongozi wa dini ya kiislamu kaunti ya Mombasa wamejitokeza kupinga kauli ya mwenyekiti wa shirika la kutetea haki za kibinadamu la muhuri aliyekuwa jaji mkuu nchini Willy Mutunga ya kuhimiza wanahabari kuunga mkono masuala ya mahusiano ya jinsia moja.
Wakiongozwa na Sheikh Abu Qatada viongozi hao walikemea hatua ya Mutunga kutetea haki na nafasi ya mahusiano na ndoa za jinsia moja humu nchini wakisema ni kinyume na maadili ya dini pamoja na katiba ya taifa.
Aidha walilitaka shirika hilo kumvua mamlaka Mutunga kama mwenyekiti wao na kutoa msimamo kuhusu suala la mahusiano ya jinsia moja huku wakitoa muda wa siku 14 kutekelezwa la sivyo watachukua hatua za kisheria.
“Tumewapatia mambo matatu wawe ni wenye kumtoa willy mutunga kama mwenyekiti wa shirika hilo,la pili wao kama MUHURI watoe msimamo wao kama shirika,ikiwa hawatoweza hayo mawili basi la tatu ambalo kwamba tutawapatia mlango wa kujisaidia wabadilishe jina la shirika lao lisiwe Muslims For Human Rights waangalie jina lingine.Wasipofanya haya matatu basi tunawapatia siku 14 tutachukua hatua za kisheria.”Alisema Abu Qatada.
Viongozi hao waliishtumu idara ya mahakama kwa kutoa uamuzi wa kuruhusu usajili wa mashirika yanayotetea mahusiano ya aina hiyo wakisema suala hilo linahujumu jitahada la kuondoa kabisa mahusiano hayo nchini na kuviweka hatarini vizazi vijavyo.
Walitoa changamoto kwa idara ya mahakama kuwa mstari wa mbele katika kulinda katiba na maadili ya taifa.
“Kauli hii inaleta mgogano na mafundisho yetu ya kidini.”Alisema Ustadh Badi.
“Tunasikitishwa pia mahakama kutoa mlango ya hawa watu kuwa wanaweza kusajiliwa kama mashirika ,ni mlango ambao kwamba tunafungua na ingongana na vitabu vya Mwenyezi Mungu na dini zote.”Alisisitiza Abu Qatada.
“Sisi tumetamaushwa sana na uamuzi wa mahakama ya upeo,unaruhusu vipi usajili wa mashirika kama hayo yanayokinzana na maadili na dini?Mtu akiletewa kotini saaii na mashtaka ya kufanya kitu kinyume na katiba ya taifa na mumewakubalia wajisajili ,how will you deal with that?Over to you Martha Koome!”Alisema Khadija Halakhe.
Haya yanajiri baada ya aliyekuwa jaji mkuu humu nchini Willy Mutunga ambaye pia ni mwenyekiti mteule wa shirika la kutetea haki za kibinadamu la MUHURI kuhimiza wanahabari kupigania haki za wakereketwa wa mahusiano ya jinsi moja mwishoni mwaka mwaka jana.