Serikali imeanzisha rasmi zoezi la uhakiki wa lazima na utoaji leseni kwa maafisa wote wa usalama wa kibinafsi –bouncers.
Katika notisi iliyowasilishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Kudhibiti Usalama wa Kibinafsi nchini Fazul Mohamed ni sharti walinzi wote wa kibinafsi wapitie zoezi hilo la uhakiki ili wapate leseni rasmi kutoka kwa serikali kabla ya kuruhusiwa kutoa huduma zozote za usalama.
Kulingana na Fazul hatua hiyo itasaidia kukabiliana na visa vya utovu wa nidhamu miongoni mwa walinzi hao.
Haya yanajiri baada ya wanahabari na maafisa kutoka Mamlaka ya Kitaifa ya Kupamabana na Matumizi ya Pombe na Dawa za Kulevya nchini NACADA kuvamiwa na walinzi wa kibinafsi wakati wa msako mkali katika Baa ya Kettle House huko Lavington Nairobi.
NACADA ilikuwa inaendesha oparesheni ya kuwanasa wauzaji wa shisha ikiwa ni hatua mojawapo ya kukabiliana na matumizi yake baada ya kupigwa marufuku nchini mwaka wa 2017.