HabariNewsSiasa

Mahakama ya Upeo Yakataa kusikiliza kesi ya Mzozo wa ardhi inayowakilishwa na Wakili Ahmednassir

Mahakama ya Upeo imeendelea kushikilia uamuzi wake wa kumpiga marufuku wakili tajika Ahmednassir Abdillahi baada ya kukataa kusikiliza kesi yake.

Mahakama hiyo sasa imekataa kusikiliza kesi ya mzozo wa ardhi ya zaidi ya shilingi bilioni 2, kesi ambayo wakili huyo anaiwakilisha familia moja dhidi ya familia ya hayati rais Daniel Moi.

Wakili Ahmednassir maarufu Grand Mulla, ambaye alipigwa marufuku na mahakama hiyo mnamo wiki jana alikuwa anapania kuiwakilisha familia hiyo lkatika kesi hiyo ya mzozo wa ardhi.

Katika kikao cha kusikiliza kesi kwa njia ya mtandao, Mahakama hiyo ikiongozwa na Jaji Mkuu Martha Koome ilisema haitaendelea kusikiliza kesi hiyo ikiwa wakili Ahmednassir atakuwa sehemu ya utetezi wa kesi hiyo, au iwapo kifaa kingine chochote cha wakili huyo kitafuatilia kikao hicho.

Kufuatia hayo mahakama imelazimimka kuahirisha kikao hicho, huku majaji 6 wakijiondoa kwenye kesi hiyo kutokana na wakili huyo kwamba atakuwa kwenye rekodi za kesi.

Itakumbukwa kuwa mnamo siku ya Alhamisi juma lililopita Mahakama ya Upeo ilimpiga marufuku Wakili Ahmednassir na kampuni yake na kesi zote anazowakilisha dhidi ya kufika katika mahakama hiyo, kwa kile walichokitaja kuwa amekuwa akiendeleza mashambulizi ya kashfa dhidi ya majaji na idara hiyo ya mahakama.

Hata hivyo Wakili huyo alijibu uamuzi huo kwa kuzidi kuukashifu na kuonesha kutojali, japo akiapa kuelekea Mahakama ya Afrika Mashariki kuupinga uamuzi huo.

BY MJOMBA RASHID