Serikali imeidhinisha kumfanyia mazishi yenye hadhi ya kitaifa mwanariadha mwendazake Kelvin Kiptum.
Katika kikao cha baraza la mawaziri kilichofanyika Ikulu ya Nairobi mnamo Jumatano, na kuongozwa naye rais William Ruto, serikali ilitangaza kuisaidia familia kusimamia gharama za mazishi ya mwanariadha huyo aliyeaga dunia katika ajali mbaya ya barabarani usiku wa Jumapili.
Kama njia mojawapo ya kumuenzi serikali itampa heshima na mazishi ya kishujaa hasa baada ya kuipa nchi hadhi na kuvunja rekodi ya dunia katika mbio za Chicago marathoni mwaka jana.
Awali kikao hicho cha Baraza la mawaziri kuliidhinisha kimya cha dakika moja kwa heshima ya mwendazake.
Haya yanajiri huku Maafisa wa Idara ya Upelelezi DCI wakianzisha uchunguzi kuhusu ajali hiyo, ambapo watu watatu tayari wametiwa mbaroni na maafisa wa polisi.
Watatu hao ni kati ya wanne wanaodaiwa kuzuru nyumbani kwa mwanariadha huyo siku kadhaa kabla ajali hiyo mbaya kutokea na kupelekea kifo chake.
Watu hao wanaodaiwa kuzuru nyumbani kwa mwendazake wakijidai kuwa maafisa wa polisi walikamatwa mapema siku ya Jumatano, na kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Iten ili kuhojiwa na maafisa upelelezi wa DCI.
Wanatarajiwa kutoa mwanga kuhusu lengo la ziara yao nyumbani kwa kina mwendazake mwanariadha huyo aliyeaga dunia kwenye ajali hiyo mbaya ya barabarani usiku wa Februari 11.
Tayari Mwili wa Kocha aliyefariki pamoja na mwanariadha huyo kwenye ajali hiyo Gervais Hakizimana ambaye raia wa Rwanda ulifanyiwa upasuaji.
Mwili wake unatarajiwa kusafisishwa kwa ndege kutoka hapa nchini hadi Kigali, Rwanda kwa ajili ya mazishi.
BY MJOMBA RASHID