HabariLifestyleSiasa

Mzozo wa Uongozi! Maendeleo ya Wanawake Mombasa wamshtumu Waziri Jumwa kuvuruga mipango yao

Chama cha Maendeleo ya Wanawake kaunti ya Mombasa Kimejitokeza kukashifu hatua ya serikali kuingilia kati uongozi na katiba ya chama hicho.

Shirika hilo lisilo la kiserikali limedai Wizara ya jinsia na tamaduni inahujumu uongozi na mikakati yake kwa kuweka viongozi ambao walikataliwa na wajumbe wanachama wao.

Katika kikao na wanahabari hapa mjini Mombasa Mwenyekiti wa Maendeleo ya Wanawake kaunti ya Mombasa, Afiya Rama alikemea vikali hatua ya Waziri wa Jinsia na tamaduni Aisha Jumwa kuendelea kupigania kurejeshwa katika shirika hilo maofisa ambao walibanduliwa uongozini kisheria.

Mwenyekiti huyo sasa anamtaka Waziri Jumwa kuheshimu katiba ya chama hicho kutatua migogoro badala ya kuhujumu umoja huo akisema kulazimisha viongozi fulani kwenye uongozi wa chama hicho ni kinyume cha sheria.

“Waziri Aisha ni mtu mkubwa sana na tunamheshimu, Hawa watu anawatetea waingie kwenye Maendeleo ya wanawake ni katiba iliwaondoa na kulingana na katiba yetu hawa watu waliotolewa wanafaa wakae kama miaka 10 kabla kurudi, lakini kufanya hivi ni kutuhujumu na sisi tunaheshimu katiba ya chama,” alisema Bi. Afiya.

Kwa upande wake Mwekahazina wa Shirika hilo mama Farida Rashid Toli amemtaka Waziri kurudi mashinani kubaini ukweli badala ya kutumia nguvu.

BY JK MAKANAKI