HabariNews

Rais William Ruto amebaini kujitolea kwa serikali yake katika kuleta mageuzi ya maendeleo ya kiuchumi nchini na kulifanya taifa kupiga hatua.

Akizungumza katika mkutano uliowaleta pamoja viongozi wa Serikali tendaji na wabunge wa mrengo wa serikali mjini Naivasha, Rais ameapa kutolegeza kamba katika ari ya kuufanya uongozi wake kuwa bora na utakaokumbukwa katika historia ya kuimarisha viwango vya maisha.

Alipuuzilia mbali wakosoaji wake wanaopinga mikakati thabiti inayotekelezwa na serikali yake akisema kuwa wanafanya hivyo ili kupata umaarufu.

Rais Ruto amekariri kuwa wana idadi kubwa ya wajumbe katika mabunge yote hivyo akiwahimiza wabunge wa Kenya Kwanza kuzingatia hoja muhimu na kupitisha ajenda za serikali bungeni.

“Tuna idadi kubwa kote katika Bunge la Seneti na la Kitaifa kusaidia kuwaimarisha nchi na kuibadilisha Kenya. Nahimiza, tufanye vile viongozi wanapswa kufanya, tushughulikie ni jinsi gani tunaweza kuimarisha nchi yetu na ni mchango gani tunaweza kutoa kulibadili taifa hili.” alisema

Amewataka wakenya kuwa na subra akiendelea kuibua mikakati ya kulibadili taifa.

Rais ruto anaongoza kikao maalum cha siku 4 cha mawaziri na wabunge wa Kenya Kwanza huko Naivasha kaunti ya Nakuru kujadili masuala tofauti tofauti na hatua zilizopigwa na serikali ndani ya mwaka mmoja.

Wakati uo huo rais alitangaza kuwa Mkataba wa kutoa nafasi za ajira laki mbili unusu kati ya taifa la Kenya na Ujerumani utaafikiwa na kutiwa saini rasmi kabla ya mwezi Juni mwaka huu.

 Rais alisema kuwa taifa hilo la Ulaya limekubali kufungua milango yake kwa Wakenya 250,000 wenye taaluma, ujuzi kamilifu n ahata wasio na ujuzi kamili katika juhudi za kuafiki mahitaji makubwa ya kazi ya Ujerumani.

Ruto aliwashauri wakenya Kuendelea kutuma maombi kupata nafasi za ajira ambazo zinatangazwa akipuuza wale wanaodai kuwa ni nafasi hewa za kazi.

BY MJOMBA RASHID