HabariNewsSiasa

Rais Ruto awarai Wakenya kushiriki utoaji maoni Kuunga Mkono Miradi ya Serikali

Rais William Ruto amesema kuwa serikali imepiga hatua kubwa katika utekelezaji wa ajenda ya maendeleo nchini katika mnamo wa mwaka mmoja uliopita.

Rais alisema kuwa serikali sasa iko katika nafasi nzuri ya kushughulikia changamoto mbali mbali zinazowakabili wakenya huku akitaja elimu za uundaji wa nafasi za ajira huduma za afya na kilimo kuwa maeneo muhimu ambayo yamepata mafanikio makubwa.

“Mwaka jana, tuliajiri walimu 56,000. Mwaka huu, tunaajiri walimu wengine 20,000 na tumeongeza bajeti ya elimu kwa Shilingi bilioni 127,” akasema.Kuhusu huduma ya afya, Rais Ruto alisema serikali imeajiri wasimamizi 100,000 wa afya ya jamii kote nchini ili kuimarisha upatikanaji wa huduma za msingi kwa wote.Alisema, Bunge limetunga sheria nne mpya za afya: Sheria ya Huduma ya Afya ya Msingi, Sheria ya Uboreshaji wa Ufadhili wa Kituo, Sheria ya Afya ya Kidijitali na Sheria ya Bima ya Afya ya Jamii ili kuharakisha utimilifu wa Huduma ya Afya kwa Wote.

Rais pia aliwataka Wakenya na taasisi mbalimbali kuunga mkono miradi ya serikali kupitia ushirikishaji wa umma na uhamasishaji.

“Tuko na mipango ya sheria mpya 4 kwa sababu tunahakikisha kuwa hakuna Mkenya atauza mali yake kulipa gharama ya hospitali. Tunataka gharama ya hospitali ilipwe kwa taratibu serikali ya Kenya itapanga.

Nawauliza wana AIPCA tuungane katika mpango huu mtoe mchngo wenu, public participation mtoe maoni yenu ndio tuweze kujua vile tutapeleka Kenya mbele kwa pamoja,” alisema.

Rais alikuwa akizungumza katika sherehe ya maadhimisho ya miaka 100 ya kanisa la Kanisa la African Independent Pentecostal Church of Africa (AIPCA) huko Kasarani jijini Nairobi.

Pia Alipongeza taasisi za dini na mchango wao mkubwa katika elimu na kuahidi kuimarisha ushirikiano kati yao na serikali.

Kiongozi huyo wa nchi pia alisema ana imani kuwa taifa la Kenya lingekuwa imara na zuri zaidi iwapo wananchi wake wangeungana na kuwa kitu kimoja.

“Wananchi wa Kenya lazima tuipende nchi hii yetu vilivyo ili kuweza kujitolea mhanga na kuweza kuifanya nchi kuwa nzuri na taifa bora, na sote tukiiungana hivyo Kenya itaenda mahali pazuri, tukishirkiana vile tumeshirikiana hii nchi itakuwa nchi inatufaa sisi sote,” alisema.

Kwa upande wake naibu wa rais Rigathi Gachagua aliwataka viongozi kuweka kando tofauti zao na kuungana mkono ili kufanya kazi pamoja kwa amani.

BY MJOMBA RASHID