HabariLifestyleNewsSiasa

Sheikh Juma Ngao kumenyana na Mwanyoha kugombea Wadhfa wa Mwenyekiti wa ODM Kwale

Sheikh Juma Ngao ameidhinishwa na viongozi wa chama cha ODM kaunti ya Kwale kuwa mgombea wa wadfa wa mwenyekiti wa chama hicho Kwale.Juma Ngao Mkuu wa Baraza la Ushauri kwa Waislamu nchini KEMNAC sasa atagombania wadhfa huo wa Mwenyekiti wa ODM na Hassan Mwanyoha ambaye ni mwenyekiti wa sasa katika uchaguzi ujao wa chama.

Wakiongozwa na Nicholas Zani viongozi hao walisema kuwa kumuidhinisha Sheikh Juma Ngao kuwa mwenyekiti kutasaidia chama hicho kuwa thabiti na kuibuka washindi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 kuanzia wadhfa wa uwakilishi wadi hadi urais.

“Tunataka kujenga ODM ikifika 2027 tupate viti vyote kutoka urais, Gavana hadi MCA. Ndio tumekubaliana sisi sote hapa Kwale kamanda wetu hapa Kwale atakuwa Sheikh Juma Ngao awe ngao ya Kwale, tunataka wanachama wajisajili kwa wingi,” alisema Bw. Zani. 

Kauli yake iliungwa mkono na Patience Lewa alisema ni sharti viongozi wa ODM wachague kiongozi aliye na maono na atakayeleta mabadiliko chamani akidai viongozi wa sasa wamefeli katika majukumu yao.

“ODM ni chama cha kitambo lakini kila uchao kunachipuka wengine wanataka kuvuruga sasa kama tulikuwa na mwenyekiti akaja na akaenda na ikiwa kumejitokeza chairman mwengine kwa nini asipewe uongozi? Kila kitu lazima kiwe na mabadiliko na ili tusonge mbele lazima tuwe na mabadiliko sasa wakati umefika tuwe imara kupata mwenyekiti wetu mpya sheikh Juma Ngao,” alisema.

Akizungumza huko Kinango katika msururu wa vikao vinavyoendelezwa na ODM kuwasajili wanachama wapya katika chama hicho, sheikh Juma Ngao alisema iwapo atachaguliwa kuwa mwenyekiti wa ODM atakomesha dhulma ambazo zimekuwa zikiendelezwa na viongozi wa sasa wa ODM wakati wa kupeana tiketi za wagombea kupitia chama hicho.

Ngao aliweka wazi kwamba baadhi ya wanasiasa hasa wanawake wamekua wakidhulumiwa kingono ili kupewa tiketi ya kuwania nyadhfa mbalimbali kaunti ya Kwale akisema atahakikisha kunakuwa na haki na usawa katika zoezi hilo.

“Tutakomesha zile dhulma za mtu apewe pesa na tikiti kisha akaanguke, na tabia za kuvua akina mama marinda ndio ampe uteuzi hiyo tutakomesha. Jambo jingine tutakomesha ni kwa baadhi ya viongozi Kwale kufanya ODM chama cha familia zao, ODM ni chama cha kitaifa si cha watu wachache au familia, hivyo tutakomesha hilo,” alisema Sheikh Ngao.Tayari wagombea wawili wamejitokeza kuwania wadhfa huo wa mwenyekiti wa chama cha ODM kaunti ya Kwale ikiwa ni pamoja na Hassan Mwanyoha ambaye ameshikilia wadhfa huo kwa miaka 15 sasa na Sheikh Juma Ngao ambaye ni mshauri wa masuala ya kidini katika kamati ya ODM nchini.

BY BINTIKHAMIS MOHAMED