Watu wawili wamefariki kufuatia ajali ya ndege iliyohusisha ndege mbili kugongana zikiwa angani jijini Nairobi.
Kulingana na ripoti ya polisi ndege ya kampuni ya Safarilink imegongana na nyengine ya kampuni ya Ninety-Nine Club ikiwa angani ilipokuwa imetoka uwanja wa ndege wa Wilson Airport kuelekea uwanja wa ndege wa Diani.
Ndege hiyo aina ya Cessna inasimamiwa na Kampuni ya Ninety-Nine Flying Club iligongana na ndege hiyo ya abiria ambapo watu wawili hao akiwemo nahodha mwanagenzi na Mkufunzi wake waliaga dunia.
Abiria 39 wa ndege ya Safarilink waliokolewa na hakuna aliyejeruhiwa huku maafisa wa ukoaji wakifika katika eneo la tukio palipoanguka ndege hizo.
Ndege hiyo ya abiria ya Safarilink hata hivyo ilirejea katika Uwanja wa ndege wa Wilson ambako ilikuwa imepaa ikiwa na abiria 44 ndani yake, 5 walikuwa wahudumu.
“Ndege hiyo ilikuwa ikienda Diani, Kusini mwa Pwani ya Kenya, ilipata kishindo kikubwa punde baada ya kuondoka uwanjani,” taraifa ya Kampuni ya ndege hiyo ilisema.
Mamlaka ya Usafiri wa Angani nchini, KCCA ilisema ajali hiyo ilitokea mwendo wa saa nne na dakika tano (10.05AM) siku ya Jumanne.
Mamlaka ya Usafiri wa Angani Nchini KCCA imetangaza kuwa wameanzisha uchunguzi wa kina kubaini chanzo cha kugongana kwa ndege hizo mbili.
Uwanja wa Wilson ni uwanja mdogo wa ndege katika jiji kuu la Nairobi ambao huwa na shughuli nyingi za usafiri hasa ukihudumikia safari za ndani.
BY MJOMBA RASHID