Muungano wa Madaktari nchini, KMPDU umeshikilia kuwa mgomo wao wa kitaifa waliopanga kuufanya juma lijalo utaanza rasmi siku ya Jumanne wiki ijayo.
Hii ni baada ya Waziri wa Afya Susan Nakhumicha kudaiwa kukosa kuhudhuria kikao cha mazungumzo kilichokuwa kimeandaliwa siku ya Jumanne, licha ya waziri huyo kutoa taarifa kwamba alikuwa tayari kwa mazungumzo.
Katika kikao na waandishi wa habari Naibu Katibu wa KMPDU, David Misekela amemshtumu Waziri Nakhumicha kwa kususia vikao, akisisitiza kuwa mgomo wao utaanza na kwamba wananchi wawe tayari kutafuta huduma katika hospitali za kibinafsi.
“Nilimsikia Waziri akisema tuje tukae mezani tuzungumze, Bi. Waziri tumekuwa kwenye meza ya mauzungumzo kwa muda wa mwaka mmoja sasa, na suala la kuajiriwa kwa madaktari Wanagenzi pia tumeweka kikao tangu mwezi Januari lakini hakuna chochote cha msingi kimezungumzwa. Hakuna chochote na tunakuambia hatupendelei kushiriki mgomo maana wagonjwa wanaumia na wananchi wanaathirika,” alisema.
Misekela aidha amedokeza kuwa madaktari wapo tayari kwa mazungumzo muda wowote kwa siku zilizosalia kabla ya makataa yao kukamilika na kinyume chake wataendeleza kitisho cha mgomo iwapo hakutafanyika mazungumzo na matakwa yao hayatachukuliwa kwa uzito.
“Katika siku saba zijazo tunapatikana usiku na mchana sehemu utakayopendekeza na uitakayo tukutane tuzungumze kuondoa huu mgomo isiwe kama ule tuliokuwa nao mara ya mwisho mwaka 2017. Hatutaki tufikia hatua kuwa tushiriki mgomo kwa masuala haya yanayoeleweka na kupaswa kushughulikiwa.” Alisema.
BY MJOMBA RASHID