HabariNews

Rais Ruto Aidhinisha Mswada wa Nyumba za Bei Nafuu kuwa Sheria

Hatimaye Rais William Ruto ameutia saini kuwa sheria Mswada wa ujenzi wa Nyumba za gharama nafuu baada ya bunge la Kitaifa la na Seneti kupitisha mswada huo wiki iliyopita.

Hii inaashiria kuwa Wakenya wote walioajiriwa watakatwa asilimia 1.5 ya mishahara yao na wale ambao hawajaajiriwa wakitoa asilimia 1.5 ya mapato yao kila mwezi kwa ajili ya mradi wa ujenzi nyumba hizo.

Akizungumza baada ya kutia saini mswada huo kuwa sheria mapema mnamo Jumanne, Machi 19 katika Ikulu ya Nairobi rais Ruto amesema mradi huo utatoa fursa kwa kila Mkenya kumiliki aina ya nyumba anayotaka.

“Katika mpango huu wa Nyumba za gharama nafuu kuna fursa kwa kila Mkenya, wale wanaotaka nyumba kubwa, za gharama nafuu, na wale wanaotaka nyumba za jamii watapata nafasi ya kuwa nazo.” Alisema

Ruto aidha alibaini kuwa mwananchi wa kawaida kama mama mboga na mwanabodaboda kuwa watanufaika vilivyo na mradi huo.

“Wengi wamekuwa wakituuliza vipi itakuwaje kwa mama mboga, wanabodaboda. Wanabodaboda wetu na mama mboga wako ndani ya mpango huu kabisa na mpango huu utamwezesha mama mboga anayelipa leo hii kodi ya 3,000 kulioa pesa hiyo na kumiliki nyumba nchini,” alisema.

Mswada huo uliofanyiwa marekebisho umetiwa saini baada ya kufanyiwa marekebisho yakiwemo kujumuishwa kwa serikali za kaunti katika utekelezaji wa mradi huo.

Hapo awali magavana kupitia vikao vya ushirikishaji maoni ya umma waliibua maswali na wasiwasi wa kwa nini serikali ya kitaifa inatekeleza mradi wa ujenzi wa nyumba hizo licha ya kuwa ni mpango uliogatuliwa.

Baada ya marekebisho na hata kutiwa saini mswada huo kuwa sheria Magavana sasa wataunda kamati za mawailiano za kaunti ili kusimamia utekelezaji wa mpango huo.

Tozo hiyo iliyoibua mgogoro kati ya Serikali, Mahakama, mashirika ya kijamii na wananchi na hata wengi kuhoji mfumo wake kisheria, sasa itatekelezwa ambapo waajiri na waajiriwa wataanza kukatwa ushuru huo mwishoni mwa mwezi huu wa Machi, baada ya kusitishwa hapo awali.

Ikumbukwe kuwa mnamo mwaka jana 2023 jopo la majaji watatu lilizuia ukusanyaji wa ushuru huo kwa msingi kwamba ulikuwa wa kibaguzi na ukiukaji wa moja kwa moja wa Kifungu cha 10 cha katiba.

BY MJOMBA RASHID