HabariNews

Utalii Waimarika; Meli ya Watalii 1,600 Yatia Nanga Bandarini Mombasa

Sekta ya Utalii ukanda wa Pwani na nchini kwa jumla imepigwa jeki na huenda ikaimarika zaidi kufuatia ujio wa meli ya Watalii ya MS Ambiens.

Meli hiyo iliyotokea Bandari ya Victoria huko nchini Ushelisheli imetia nanga bandarini Mombasa mwendo wa saa 5.30 Alfajiri ya Jumatano Machi 27, ikiwa na watalii 1,600.

Meli hiyo illiyokuwa na abiria 1,100 na wafanyakazi 500 sasa inaongeza idadi ya meli za watalii zilizotia nanga Mombasa mwaka huu kuwa nne.

Akizungumza baada ya kuwapokea watalii hao Katibu katika Wizara ya Utalii John Olol’tua alibaini kuwa jumla ya watalii 8,366 kufikia sasa wamezuru taifa hili kupitia safari za baharini hatua inayozidi kuimarisha uchumi na mapato ya sekta hiyo.

Tangu mwezi Januari mwaka huu 2024 tumepokea jumla ya Meli 4 za Watalii zikiwa na abiria pamioja na wafanyakazi kwa jumla wakiwa 8,366 kufikia sasa. Na hili linaashiria kuwa Kenya ni mojawapo ya Vituo vikuu vya safari za kitalii za meli barani Afrika.” Alisema.

Olultua amesema watalii hao watazuru maeneo mbalimbali nchini ikiwemo ziara ya hapa Mombasa na mbuga za wanyama za Tsavo na Amboseli, akisema kuwa ujio huo wa meli unaashiria kuwa Kenya ni mojawapo ya Sehmu kuu za safari za Watalii Baharini hapa barani Afrika.

Ndani ya siku mbili watakazokuwa hapa nchini watafanya ziara ya mji huu wa Mombasa na pia watazuru Tsavo na Amboseli na katika mchakato huo kweli athari za uchumi wa sekta hii kukua itakuwa kubwa sana.” Aliongeza.

Egil Eyune ni nahodha wa Meli hiyo na anasema kampuni hiyo ya meli ina miaka miwili sasa na ni mara ya kwanza kufanya ziara yake kwa mataifa mbalimbali ambapo baada ya ziara ya Kenya itaelekea bandari ya Durban, Afrika Kusini kisha kuelekea Brazil Marekani Kusini kabla ya kumalizia safari yake London.

BY NEWS DESK