Waziri wa afya kaunti ya Kilifi huenda akalazimika kufika katika bunge la kaunti ya Kilifi kuelezea sababu ya ongezeko la visa vya wanawake wajawazito kufariki dunia wakati wa kujifungua licha ya juhudi nyingi kufanywa kuhakikisha kuwa hakuna mwanamke yeyote anayepoteza maisha kutokana na uzazi.
Idadi ya wanawake kuaga dunia wakati wa kujifungua inaripotiwa kuongezeka katika wadi ya Tezo eneo bunge la Kilifi kaskazini, zaidi ya visa vitatu vya mama na mtoto wakifariki dunia vikiripotiwa ndani ya mwezi mmoja.
Kulingana na diwani wa Tezo Thomas Chengo aliyepia kiongozi wa wachache katika bunge la kaunti ya Kilifi, ni jambo la kusikitisha kuona kwamba familia zinakumbwa na hali ya wasi wasi pindi mpendwa wao anapokwenda kujifungua hospitalini.
Amesema swala hili linafaa kushughulikiwa kwa uzito mkubwa na kwa haraka ili kunusuru wanawake walio katika hatari ya kupoteza maisha yao wanapozuru vituo vya afya kujifungua.
“Kina mama wanapoenda kujifungua asilimia kubwa tunaona kwamba kuna hatari ya kwamba huenda wakapoteza maisha. Labda yeye ama yule mtoto ama wote wawili. Na mimi binafsi katika wadi yangu ya Tezo, kuna visa kadha wa kadha ambavyo nimevishuhudia ikiwemo kisa cha jana mama alienda kujifungua na wote wawili wakapoteza maisha.
“Na hata hivi leo kuna mwengine Kaereni anazikwa na hali ni hizo hizo za uzazi kwa hivyo ni swala ambalo si la kuangaliwa kwa jicho la huruma ni swala ambalo ni liangaziwe kwa ukakamavu, ili tuone kina mama wanapokwenda pale kuna usalama wa kutosha.” alisema Chengo.
Vile vile ameeleza kuwa atafuata hatua hitajika ili kuhakikisha kwamba waziri wa afya kaunti ya Kilifi anafika katika bunge la kaunti ya Kilifi kujibu sababu ya ongezeko la visa hivyo vya wanawake kufariki dunia wakati wa kujifungua.
“Nikiwa kiongozi lazima nifuatilie nihakikishe kuwa idara husika inawajibikiaje swala hili iwapo limetokea kwa mara ya kwanza na kwa mara ya pili. Na nikisema kwamba tutaweza kumuita waziri sio kumuita tu nimetoa haya maelezo kwasababu ya uchungu na kwasababu ya kwamba wananchi wanashuhudia haya yanayotokea.
“Tutafuata zile sheria zinazohitajika bungeni kuona kwamba ameweza kufika na kutuelezea ni kwanini maswala haya yanatokea na hatujaona chochote akitueleza kwa ajili ya kuchukua hatua za kutatua swala kama hili.” alisema Chengo.
Hayo yanajiri huku serikali ikiendeleza hamasa kwa wanawake wajawazito kufika hospitalini wanapotaka kujifungua.
ERICKSON KADZEHA