HabariMombasa

Asilimia 80 ya visa vya dhulma za kijinsia kwa watoto wadogo vinatokana na ngono…

Imebainika kuwa asilimia 80 ya visa vya dhuluma za kijinsia kaunti ya Mombasa vinatokana  na vitendo vya ngono kwa watoto wa kike na wa kiume walio chini ya umri wa miaka 18 huku asilimia 90 wakiwa watoto chini ya umri wa miaka 10.

 

Haya ni kwa mujibu wa mratibu wa masuala ya dhulma za kijinsia kwa masuala ya ngono katika gatuzi dogo la Likoni Stephen Kalai.

 

Akizungumza katika hafla ya kutoa hamasa kwa jamii kuhusiana na masuala ya dhulma za kijinsia pamoja na maradhi ya kiakili katika hospitali ya gatuzi dogo la Likoni,Kalai amesema miongoni mwa watu wanaohusika na visa hivyo ni watu wanaoheshimika katika jamii na wala si mateja wala watu wenye akili punguani kama vile wengi wanavyodhania.

 

Akiangazia suala la ugonjwa wa kiakili mbunge wa Mvita Abdulswamad Shariff Nassir amesema, kulingana  na takwimu kutoka kwa shirika la Kenya Bureau Of Statistics kiwango cha ugonjwa wa akili ni moja wapo ya kiwango cha juu zaidi hapa nchini.

Haya yanajiri huku ripoti ya mwaka 2020 iliyotolewa na mashirika ya kutetea haki za binadamu likiwemo Haki Afrika ikionyesha kuwa visa 771 vya dhuluma ya kijinsia viliripotiwa kutoka maeneo mbali mbali kanda ya pwani mwaka wa 2020 ukiliganisha na mwaka wa 2019 ambapo visa 76 pekee viliripotiwa.