HabariMazingira

Wazee huko Kilifi sasa wataka barabara kuu ya Malindi – Mombasa kufanyiwa tambiko….

Muungano wa Sauti ya wazee wa mijikenda maeneo bunge ya Malindi na Magarini kaunti ya Kilifi sasa wanamtaka Gavana wa kaunti hiyo Amason Jeffah Kingi kushirikiana nao na kupanga siku maalum ya kufanya matambiko katika sehemu ambayo imekuwa ikishuhudiwa ajali za barabara huko Kizingo.

Wakiongozwa na Johnson Charo Hinzano na Luwali Fondo Birya wazee hao wanadai eneo hilo linafaa kufanyiwa maombi maalum haraka iwezekanavyo baada ya kushuhudiwa msururu wa ajali katika muda wa siku chache.

Kulingana na wazee hao kuna haja ya uongozi wa kaunti hiyo kuliangazia swala hilo kwa undani zaidi wakidai si jambo la kawaida katika mila na desturi za kimijikenda.

Kwa upande wake katibu mkuu wa chama hicho Simon Garama Mvundi anaitaka serikali kujizatiti katika kufuatilia miradi tofauti tofauti kwa wanakandarasi wanaosimamia.

Mvundi aidha amesisitiza haja ya Gavana Kingi kufuatilia kwa karibu miradi ya serikali ya kitaifa ili kuhakikisha inaendeshwa kwa ufasaha.

Kauli ya wazee hao inajiri huku ajali nyengine ikifanyika maeneo hayo japo hakuna majeruhi yaliyoshuhudiwa.