Habari

Jaji wa mahakama ya uajiri na Leba Mathew Nduma Nderi ndio wa kwanza kuhojiwa wiki hii…

Jaji wa mahakama ya uajiri na Leba Mathew Nduma Nderi ndio wa kwanza kuhojiwa wiki hii na makamishna wa tume ya huduma za mahakama JSC  katika mahojiano ya kumtafuta jaji mkuu mpya na mwenyekiti wa tume ya huduma za mahakama JSC yaliyoanza wiki iliyopita.

Katika mahoajiano hayo yanayoendelea jaji Nduma ametakiwa kueleza kuhusu kauli yake kwamba taifa linahitaji jaji mkuu mwenye uadilifu  na mwenye uwezo wa kutoa uamuzi bila ya kuegemea upande wowote.

Amesema jaji mkuu anahitaji kuwashirikisha wenzake katika maamuzi yote yanayofanywa ili kurahisisha shughuli ya utoaji wa haki.

amesema idara ya mahakama inapaswa kukumbatia mfumo wa kuwasilisha kesi kupitia mitandao ikiwemo utoaji wa uamuzi kielektroniki ili kupunguza mrundiko wa watu wanaotafuta haki mahakamani.

wakati huo huo Jaji Nderi amepuzilia mbali madai kwamba yeye ni jaji wa kukasirika haraka na si mtu wa kutangamana.

Kuhusu uamuzi wa Maraga kufutilia mbali ushindi wa rais Kenyatta mwaka 2017, kutokana na madai ya wizi wa kura, Jaji Nderi anasema angefuata sheria na iwapo ushahidi wa kutosha ungewasilishwa mbele yake bila shaka angetoa maamuzi yayo hayo.

Jopo hilo la JSC linaongozwa na proffesa Olive Mugenda ambaye ni mwenyekiti wa sasa.

Jaji Nduma Nderi ni miongoni mwa majaji watano walioratibiwa kuhojiwa wiki hii, ambapo wakili Fred Ngatia atahojiwa hapo kesho, jaji wa mahakama ya rufaa William Ouko atakayehojiwa jumatano miongoni mwa wengine wawili waliosalia.

Jaji Nderi mwenye umri wa miaka 59 ana uzoefu wa zaidi ya miaka 31 katika sekta ya uanasheria huku sehemu kubwa ya uzoefu huo akiupata nje ya nchi.