HabariSiasa

Seneti kuendeleza kikao cha kujadili mswada wa BBI saa nane unusu alasiri leo…

Bunge la seneti limelazimika kuahirisha kikao maalum cha kujadili ripoti ya mswada wa marekebisho ya katiba wa mwaka 2020 hadi saa nane na nusu alasiri ili kuwapa muda maseneta kusoma Ripoti hiyo iliyoandaliwa na kamati ya pamoja ya haki na sheria JLAC kuhusu mswada huo.

Seneta wa BUNGOMA Moses Wetangula na mwenzake wa Siaya James Orengo ni miongoni mwa maseneta waliotaka kupewa muda zaidi ili kuweza kufahamu zaidi yaliyo kwenye ripoti hiyo.

amesema watakapoifahamu ripoti hiyo wataweza kufanya uamuzi wa busara wakati wa kupiga kura.

Kwa upande wake bunge la kitaifa linatarajiwa kujadili ripoti hiyo ya mswada wa marekebisho ya katiba katika kikao cha alasiri leo.

Mwenyekiti wa kitaifa wa chama cha ODM John Mbadi amesema katika vikao vya asubuhi watajadili masuala mengine ikiwemo mswada wa ugavi wa mapato, ambao seneti waliupitisha huku bunge hilo likipendekeza mabadiliko kadhaa.

Mbadi anasema huenda kura kuhusu mswada wa marekebisho ya katika ikapigwa wiki ijayo na bunge hilo.

Licha ya kuwepo kwa hisia tofauti kuhusu mswada huo, Mbadi anasema kizingiti kikuu katika kufanikisha kura ya maamuzi ni mahakama, kwani kesi mbali mbali zimewasilishwa kupinga mchakato huo.

By Warda Ahmed