Habari

ALIYEKUWA MWAKILISHI WA WANAWAKE KATIKA KAUNTI YA KWALE BI ZAINAB CHIDZUGA AAGA DUNIA …………..

Aliyekuwa mwakilishi wa wanawake katika kaunti ya Kwale Bi Zainab Chidzuga ameaga dunia mapema mchana wa leo.

Kulingana na familia ya mwendazake tuliozungumza nao, Mwendazake alikuwa amelazwa katika hospitali ya Nairobi jijini Nairobi kwa muda wa wiki mbili baada ya kuugua maradhi ya Covid 19.

Viongozi mbalimbali wa wametuma salamu zao za rambirambi  kufuatia kifo cha kiongozi huyo.

Wakiongezwa na rais Uhuru Kenyatta na naibuw wa rais William Ruto, viongozi hao wamemtaja mwendazake kuwa mkakamavu,mpenda watu na mchapa kazi pamoja na kuwa  mtetezi wa wanawake kwa kuwa mstari wa mbele  katika kupigania haki na miradi ya wanawake katika kaunti ya Kwale na nchini kwa ujumla, huku akiwa mwanzilishi wa shirika la Maendeleo ya Wanawake ya MYWO.

Wakati huohuo Viongozi mbalimbali kaunti ya kwale ,wakiongozwa na Gavana wa kwale salim mvurya, Mbunge wa msambweni Feisal Bader,mwakilishi wa kinamama kwale zuleikha Hassan wanamtaja mwenda zake aliyekuwa kiongozi shupavu tangu alipoanza safari yake ya kisiasa.

Wakaazi wa kaunti ya Kwale wamekiri kuwa pigo kwao haswaa kama kiongozi na mtetezi wa wanawake katika kaunti hiyo.

Mwendazake aliyefariki akiwa na umri wa miaka 65 ameacha watoto 6

Zainabu chidzuga amekuwa mkurugenzi wa bodi ya unyunyiziaji na mwenyekiti wa maendeleo ya wanawake pwani.

Hadi kufa kwake amekuwa mwana chama wa jubilee baada ya kukihama chama  ODM.

Mwili wa mwendazake unatarajiwa kusafirishwa hadi kaunti ya Kwale ambako anatarajiwa kuzikwa.

Chidzuga aliwakilisha wakaazi wa Kwale mwaka 2013 hadi 2017.