HabariKimataifaNews

Kundi la kwanza la wakimbizi 51 wa Afghanistan lawasili Uganda…

Taarifa ya Wizara ya mambo ya nje nchini Uganda imesema kwamba Kundi la kwanza la wakimbizi 51 wa Afghanistan limewasili katika uwanja wa kimataifa wa Entebbe kupitia ndege binafsi.

Wizara hiyo imeongeza kuwa kundi hilo linapita tu Uganda na litaelekea Marekani na nchi nyingine, ingawa haijafahamika kundi hilo litakaa Uganda kwa muda gani.

Taarifa hiyo aidha imesema watu hao walifanyiwa vipimo vya virusi vya korona na kwamba watakaa karantini.

Uganda imepokea watu hao kufuatia maombi ya serikali ya Marekani ya kutaka nchi hiyo isaidie kupokea watu wanaokimbia ghasia za Afghanistan tangu kundi la Taliban lishike hatamu juma lililopita.

Wiki iliyopita serikali ya Uganda ilisema kwamba nchi hiyo inatarajia kupokea wakimbizi 2,000 kutoka Afghaistan kutokana na maombi ya Marekani, Lakini maafisa wa juu wa serikali baadae walisema kwamba mazungumzo bado yanaendelea.

Uganda inawahifadhi wakimbizi zaidi ya milioni 1 kutoka nchi za ukanda wa Afrika Mashariki ambao wamekimbia nchi zao kwa sababu ya vita na majanga mengine.

BY NEWS DESK.