AfyaHabariNews

Serikali yapanga Mikakati ya kukabiliana na Mkurupuko wa Magonjwa Kufuatia Mvua Kunyesha

Athari za mafuriko zikiendelea kushuhudiwa maeneo tofauti humu nchini kufuatia mvua kubwa kunyesha, serikali imeweka mikakati yakukabiliana na mkurupuko wa magonjwa na visa kadhaa vya ugonjwa wa kipindupindu vilivyoripotiwa.

Serikali inaendelea kukamilisha mikakati ya kukabiliana na mkurupuko wa magonjwa kufuatia maeneo mengi ya nchi kushuhudia mafuriko kutokana na mvua kubwa.

Kulingana Waziri wa afya nchini Susan Nakhumicha, serikali ya kitaifa tayari imeanza kusambaza dawa pamoja na vifaa mbali mbali vitakavyosaidia kukabiliana na athari za mvua inayoendelea kunyesha.

Alieleza kuwa kaunti ya Kilifi ilipokea dawa za shilingi milioni 5.8, na vyandarua vya kuzukijinga mbu elfu 5 miongoni mwa vifaa vingine ili kukabiliana na athari hiyo.

“Tumeleta dawa, tunajua msimu huu kutakuwa na magonjwa mengi sana kwa hivyo serikali ya kitaifa tumeleta dawa za kima cha shilingi milioni 5.8 kwasababu tunataka kuhakikisha kwamba tunakinga ugonjwa tumeleta pia dawa za kudhibiti uambukizaji zenye thamani ya shilingi nusu milioni, nyumba, na maeneo yanayokwama maji yaweze kunyunyiziwa ili kuzuia watu wetu dhidi ya magonjwa. Pia tumeleta vyandarua vya kujikinga mbu elfu 5” alisema Nakhumicha.

Kwa upande wake naibu gavana wa Kilifi Florence Mbetsa, wakazi 21 wamefariki dunia kutokana na kushuhudiwa kwa mvua kubwa kaunti ya Kilifi, akiongeza kuwa familia zaidi ya 400 zikinusuriwa na balaa la mafuriko huku akielezea hofu yake kwamba huenda mkurupuko wa maradhi ukaanza kushuhudiwa siku chache zijazo.

“Kaunti ya Kilifi ni miongoni mwa kaunti zilizoathirika zaidi na mvua kubwa iliyoshuhudiwa, jumla ya nyumba 796 ziliharibiwa, huku watu 434 wakinusuriwa na kupelekwa kwenye kambi tofauti tofauti. Mafuriko hayo yametugharimu maisha ya watu 21 huku wengine wawili wakiachwa na majeraha mabaya.” alisema Mbetsa.

Ikumbukwe tayari watu watatu wameripotiwa kufariki dunia kaunti ya Lamu, kutokana na ugonjwa wa kipindupindu.

BY ERICKSON KADZEHA