HabariMakalaNews

Press Clubs; Uzinduzi wa Afisi na Miungano ya Wanahabari wa Pwani kutatua Changamoto za Waandishi

Wanahabari eneo hili la Pwani wameanzisha mchakato wa kuunda muungano wa wanahabari katika kila kaunti maarufu Press Club ili kushughulikia zaidi maslahi yao na changamoto mbalimbali zinazowakabili.

Hatua hii inajiri kufuatia changamoto za waandishi habari kukosa afisi na mazingira bora ya kufanyia kazi.

Kaunti ya Kilifi ilikuwa ya kwanza eneo la Pwani kuzindua Klabu ya wanahabari mnamo siku ya Jumanne Januari 30, hafla iliyoongozwa na Afisa Mkuu Mtendaji wa Baraza la wanahabari nchini (MCK) David Omwoyo na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali.

Katika halfa hiyo wanahabari walibaini kuwa wamekuwa wakipitia changamoto nyingi ambazo zimelemaza kuafikiwa kwa malengo yao.

Mwenyekiti wa Muungano huo wa Wanahabari wa Kilifi Elias Yaa na alieleza kuwa lengo la kubuniwa kwa muungano na afisi hiyo ni kuleta pamoja wanahabari na kuimarisha utendakazi wao sawia na suluhisha changamoto zinazowakbili.

“Tumekuwa tukipitia changamoto nyingi kama waandishi nyanjani, na hii Kilifi Press club tuna mikakati mingi na kwanza ni kubuni ofisi ya Media hub ambako itakuwa sehemu ya mwanahabari yeyote aliyeidhinishwa na MCK anaweza kufika na kufanyia kazi hapo, na tunashirikiana na Baraza la wanahabari MCK kuona hili tunalitimiza,” alisema.

Aidha wanahabari hao wameitaka mashirika ya wanahabari yenye makao yake makuu jijini Nairobi kushirikiana na wanahabari wa kaunti ya kilifi ili kutimiza lengo lao la kupata habari.

Huko kaunti ya Kwale Klabu ya wanahabari ilizunduliwa rasmi kama njia moja wapo ya kuimarisha na kukuza vipaji vya wanahabari chipukizi na kuinua taaluma zao.

Akiongea katika uzinduzi huo Afisa Mkuu mtendaji wa Baraza la Wanahabari nchini MCK, David Omwoyo alisema vikundi hivyo vya wanahabari kutoka kaunti tofauti tofauti ni vya kuimarisha utendakazi na kuwawezesha waandishi kiuchumi na hata kukuza talanta zao za uandishi.

“Vikundi hivi vitawasaidia waandishi wa kaunti hizi kuboresha utendakazi, kujiinua kiuchumi na kuendeleza talanta zao,” alisema Bw. Omwoyo.

Naibu Gavana wa Kwale Chirema Kombo aliyehudhuria hafla ya uzinduzi huo aliwataka wanahabari kuunda kampuni itakayowawezesha kupata zabuni na kandarasa za kuwapa fedha za kujiinua kiuchumi.

Naye Naibu Msemaji wa Serikali Mwanaisha Chidzuga ambaye aliwahi kuhudumu kama mwanahabari hapa Pwani na kitaifa aliwahimiza waandishi kuwa makini zaidi kazini na kuzingatia usalama wao huku akiwaahidi kushirikiana nao katika kuendeleza kikundi hicho na taaluma zao.

“Niwahimize mzidishe ushirikiano huu lila muwe makini mnakpokuwa kazini mzingatie usalama wenu zaidi maana hakuna taarifa iliyo bora zaidi ya maisha yako, lakini taaluma na kanuni zizingatiwe. Tutashirikiana kuendeleza klabu hii.” Alisema

Haya yanajiri huku mikakati ya kubuni miungano na klabu za wanahabari ikiendelezwa katka kaunti mbalimbali Pwani na kote nchini.

Katika kaunti ya Mombasa mikakati na harakati za kuzindua rasmi klabu yao inaendelezwa wanatarajiwa kuzindua Muungano huo katika siku za hivi karibuni.

BY OUR REPORTERS