HabariNews

Wabunge Kukatiza Likizo; Kurejea Bungeni Kuamua Hatma ya Waziri wa Kilimo

Wabunge wameagizwa kutoka likizoni ili kufanya kikao maalum wiki ijayo cha kuamua hatma ya Waziri wa Kilimo Mithika Linturi.

Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangula amewaagiza wabunge kurejea kwa ajili ya kikao hicho kitakachofanyika Jumatatu ijayo, Mei 13, ambapo bunge litapokea ripoti ya uchunguzi kuhusu utendakazi wa Linturi.

Spika Wetangula amesema ajenda kuu ya kikao hicho ni kuzingatia ripoti ya kamati teule iliyotwika jukumu la kuchunguza madai ya kumwondoa mamlakani waziri Linturi.

Kamati teule ya wajumbe 11 inayoongozwa a Mbunge mwakilishi wa wanawake wa Marsabit Naomi Wako ilianza vikao vyake Alhamisi wiki jana kujadili madai yanayomkabili waziri Linturi.

Waziri huyo anatarajiwa kupewa nafasi ya kujitetea bungeni dhidi ya tuhuma zinazomkabili zikiwemo matumizi mabaya ya afisi hasa baada ya kuhusishwa na Sakata ya Mbolea ghushi.

Katika kikao hicho cha dharura Bunge la Kitaifa pia linatarajiwa kujadili mswada muhimu unaolenga kuimarisha juhudi za serikali na namna serikali za kaunti nay a kitaifa zinapaswa kukabili athari ya majanga yanayoshuhudiwa.

Katika mswada huo kunakusudiwa kuundwa baraza maalum la serikali la kusimamaia majanga sawia na kuundwa kwa mamlaka itakayosadiana na baraza hilo, mamalaka ambayo itakuwa na ofisi yake maalum.

 Kulingana na kalenda ya Bunge ni kwamba wabunge walianza likizo Alhamisi iliyopita na walifaa kurejelea vikao vyao bungeni mnamo Juni 4.

 BY NEWS DESK