HabariLifestyleNews

Inspekta Jenerali Ataka Washukiwa Wazuiwe Kuvaa Barakoa wanapofika Mahakamani,

Inspekta Jenerali wa Polisi Japhet Koome sasa anapendekeza kupigwa marufuku uvaaji wa barakoa, sweta au makoti yenye kofia, na miwani za kuficha mwonekano wa sura ya mtu kwa washukiwa wanaofikishwa mahakamani.

Akizungumza mjini Mombasa wakati wa Kongamano la Kukabiliana na Pombe haramu na mihadarati, siku ya Jumatatu Koome alisema washukiwa wanafaa kupitia udhalilishaji kwa kuacha sura zao zionekane na kila mmoja ili kuwakatisha tamaa wengine ambao wanaweza kujiingiza katika shughuli ambazo washukiwa wanashtumiwa nazo.

“Tumeruhusu washukiwa kuvaa barakoa koritini kwa muda mrefu sasa; wanavaa maski, miwani kubwa na maboshori ya sweta kiasi cha kutoona sura zao. Inabidi tufikiria upya haya,” alisema.

Koome ambaye alikuwa akihutubia washikadau akiwemo rais William Ruto, Naibu wake Rigathi Gachagua na Waziri wa usalama wa Ndani Prof. Kithure Kindiki, alisisitiza kuna haja ya kubadili mtazamo na mbinu za kutekeleza mambo, sawia na kuwa na msimamo mkali katika hilo ili kuleta mwanga wa vita dhidi ya mihadarati.

Tunahitaji kuwaona, angalau kuna adhabu ya kuonekana na kila mtu…wanahitajia kuaibishwa Mheshimiwa Rais, lazima tubadili namna tumekuwa tukifanya mambo, tuwe na msimamo mkali ikiwa tunataka kubadili jamii,” alisema.

Alisema Vijana katika eneo hili wamejiingiza katika lindi la mihadarati na ‘hawajali kamwe.’

Wakati uo huo Koome aliwashtumu Wakuu wa usalama kaunti ya Mombasa kwa kusita kuwakamata walanguzi na wafanyabishara wa mihadarati.

Aliwapa muda wa siku nne kukamata angalau mtu mmoja anayeshtumiwa kuendeleza ulanguzi wa dawa za kulevya katika ebeo hili.

Kwa muda mrefu, hamjakamata mlanguzi wa mihadarati. Nipo hapa kikazo kwa taribani siku nne. Lazima tupate Mlanguzi ndani ya siku hizi, hamna chaguo,” alisema Koome.

BY MJOMBA RASHID