HabariNews

Naibu Spika wa Bunge la Taita Taveta Aachiliwa kwa Dhamana ya Sh. Milioni 1

Mahakama ya Mombasa imemwachilia kwa dhamana Naibu Spika wa bunge la Kaunti ya Taita Taveta Anselm Mwadime Chao.

Mwadime aliyekamatwa na maafisa wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi-EACC, mnamo siku ya Jumapili ameachiliwa kwa dhamana ya shilingi milioni moja au pesa Taslim shilingi 500,000.

Mwadime amesomewa mashtaka mawili makuu yanayomkabili ya ubadhirifu wa fedha za umma na utumizi mbaya wa ofisi, ambapo anadaiwa kuidhinisha malipo ya shilingi milioni 7 kwa wawakilishi wadi kusafiri hadi Kisiwani Zanzibar kinyume cha sheria.

Shtaka jingine ni kuidhinisha malipo ya shilingi milioni 1,346,870 kinyume cha sheria kwa maafisa watano wa idara ya ukatibu katika Bunge la Kaunti hiyo kati ya Oktoba 2022 na Novemba 2022.

Kadhalika naibu huyo wa spika anatuhumiwa kuhusika katika matumizi mabaya ya shilingi 795,675 ambazo zililipwa kinyume na sheria kwa Chrispus Tondo, Rose Sariki na Mohammed Omar waliohudhuria mafunzo nchini Zanzibar licha ya wao kutokuwa wanachama wa kamati kuu ya Bunge hilo.

Akiwa katika mahakama ya Mombasa inayosikiliza na kutoa hukumu ya kesi za ufisadi Mwadime hata hivyo ameyakana mashtaka yote yaliyosomwa dhidi yake na hakimu Alex Ithuku.

Kesi hiyo inatarajiwa kutajwa tena Machi 11, 2024.

BY ISAIAH MUTHENGI