HabariNews

Mbona Mmenyamaza? Naibu Rais Awasuta Viongozi Pwani Kwa Kufumbia Macho Tatizo la Mihadarati

Naibu Rais Rigathi Gachagua ameibua maswali kuhusu ukimya wa viongozi waliochaguliwa eneo la Pwani katika masuala ya dawa za kulevya.

Akiongea mnamo Jumatatu, Februari 26 wakati wa Kongamano la Kupambana na Pombe haramu na dawa za kulevya mjini Mombasa Gachagua alihoji kimya cha viongozi hao katika vita dhidi ya mihadarati inayoendelea kuangamiza wakazi eneo hili.

“Kwa nini viongozi wa Pwani wamenyamaza huku idadi ya vijana wetu ikiuawa na kuangamizwa na dawa za kulevya? Kuna janga kubwa Pwani, na uongozi umenyamaza. Angalau nimemsikia Moha (Mbunge Nyali) na Ruweida (Mbunge Lamu Mashariki),” alisema Gachagua.

Naibu huyo wa rais aidha alionyesha kutoridhishwa na hatua ya viongozi wengi wa ukanda wa Pwani kukosa kuhudhuria kongamano hilo akihoji uwajibikaji wao katika janga hilo lililoangamiza maisha ya maelfu ya vijana wengi.

“Kwa nini wengine hawako hapa? Kuna kongamano muhimu kujadili uwepo wa idadi ya watu wetu hapa. Huu ni mjadala ambao kila kiongozi aliyechaguliwa anafaa kuwa miongoni na sehemu ya mjadala kwa sababu ni tatizo kubwa,” aliongeza Gchagua.

Wakati uo huo Gachagua aliwakashifu viongozi wa Pwani kwa kuonyesha utepetevu katika kukemea uozo huo ikilinganishwa na viongozi wengine hasa wa eneo la Bonde la Ufa katika kukabiliana na mihadarati.

“Labda viongozi wanatuambia hakuna tatizo. Inatia wasiwasi sana na tuna hofu kama serikali,” alisema.

Aliwataka viongozi kuunda ushirikiano wa pamoja na idara za kiusalama katika eneo hili ili kusaidia kukabiliana na utumizi wa mihadarati.

BY MJOMBA RASHID