HabariMombasaNews

WAKAZI WAHIMIZWA KUZINGATIA ELIMU NA UKULIMA KUIMARISHA MAISHA KILIFI.

Wakazi kaunti ya Kilifi wamehimizwa kuzingatia zaidi maswala ya elimu na ukulima ili kujiimarisha maishani, pamoja na kuweka msingi bora wa maisha ya baadae kwa vijana kaunti hiyo.

Wakazi kaunti ya Kilifi wameshauriwa kuzingatia swala la elimu na ukulima kama njia ya kujiimarisha maishani lakini pia kuwawezesha kuwasomesha wanawao.

Akizungumza mjini Kilifi wakati wa hafla ya kupeana hundi za ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza, mbunge wa Kilifi kaskazini Owen Baya amewasistiza wazazi kujihusisha na ukulima ili wanapouza mavuno waweze kuwalipia watoto wao karo na vile vile pia kupata chakula.

Amesema muda umefika sasa kwa wakazi kukoma kuuza mashamba ili kulipa karo za shule badala yake wawekeze kwenye mashamba hayo ili kuimarisha mavuno yatakayowapa fedha baada ya kuyauza.

“Kuna mambo mawili ambayo ni muhimu, elimu na ukulima. Elimu itafukuza umasikini baadae motto kama amemaliza. Lakini sasa huu umasikini tutaufukuza vipi? Lazima turudi mashambani tulime. Na huu ukulima tukiushika vizuri tunasema hakuna kazi sivyo, lakini huu ukulima tukiushika industries zitakuja  kutengeneza nafasi za kazi, na watakao ajiriwa ni vijana wetu lakini lazima tufanye bidii” alisema Baya.

Aidha amewataka wazazi kujukumika zaidi katika kuhakikisha kuwa wanao wanapata elimu kwa kujitahidi kulipa karo.

Ameeleza kuwa mgao wa fedha za ufadhili wa masomo hauwezi kutosheleza kusimamia masomo ya wanafunzi wote huku akiwataka wazazi kutowaachia wabunge jukumu la kuwalipia karo wanao.

“Sasa mimi nataka niwaambie ndugu zangu hili jukumu la kusomesha mtoto ni letu haya maneno ya barsury iwe ni usaidizi. Tukijua kujisaidia na kutafuta hawa watoto hawatatushinda. Mimi pia naamini kama vile wanaamini Wakristo kwenye Biblia Mungu hawezi kukupatia mzigo mzito ukushinde, lakini mpaka ukubali huo mzigo mwanzo, halafu ufanye bidii ndio mzigo utakuwa rahisi”. alisema Baya.

Hayo yamejiri wakati wa kutoa hundi za ufadhili wa masomo ambapo zaidi ya shilingi milioni sita zimetolewa kwa wanafunzi wanapojiandaa kurudi shuleni kwa muhula wa pili.

 

ERICKSON KADZEHA