HabariLifestyleMombasaNews

Serikali ya Kaunti ya Mombasa Yatangaza azma ya Kuwalipa Mishahara Walimu wa Madrassa

Serikali ya kaunti ya Mombasa imetangaza mpango wa kuzindua malipo kwa walimu wa madrasa katika kaunti hiyo.

Akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa msikiti wa Shariff Ali eneo la Ganjoni hapa Mombasa, Gavana wa Mombasa Abdulswamad Shariff Nassir alisema Serikali yake imeweka mikakati ya kuwaeka kwenye orodha ya malipo ya kila mwezi akibaini kuwa walimu hao watalipwa kama vile serikali ya kaunti inavyowalipa walimu wa shule za chekechea.

Kulingana naye walimu wengi wa dini wamekuwa wakijitolea kufundisha bila ya malipo akisema mpango huo utawasaidia pakubwa katika kuwatia nguvu ya kutekeleza kazi zao vyema.

“Nitalipeleka katika Bunge liweze kuorodheshwa hili. Si vibaya walimu wetu wa madrasa walipwe kama walimu wa ECDE, itakuwa imeweza kuondoa dhiki na watoto wetu waingie katika mpangilio huu kupata elimu, ni jambo ambalo kwamba nalipika niombeeni Mungu hili kama vile mengine yalishaiva na hili litaiva inshaAlah,” alisema Nassir.

Aidha akizungumza katika hafla tofauti ya kuwatuza watahiniwa wa kidato cha nne katika shule ya upili ya wasichana ya Shariff Nassir, Gavana Nassir amesema Serikali ya kaunti ya Mombasa inapanga kutoa ufadhili wa karo kwa watahiniwa bora wa kidato cha nne waliomaliza mtihani wao wa KCSE mwaka jana ili kujiunga na vyuo vikuu.

Alisema kuwa kila mtahiniwa bora wa shule za kutwa za umma kaunti ya Mombasa atapata ufadhili wa karo ya shilingi elfu 50 kila mmoja ili kujiunga na vyuo vikuu.

Kuhusu masuala ya siasa Gavana Nassir amewataka walio kwenye mamlaka kuepuka kusutana katika majukwaa ya kisiasa.

Kwa mujibu wa gavana Nassir huu ni wakati wa kuwahudumikia wananchi wala sio wa kusutana katika majukwaa.

 

BY NEWSDESK