HabariNews

Joseph ‘Jowie’ Irungu Ahukumiwa Kifo kwa Kesi ya Mauaji iliyomkabili

Mahakama kuu imemhukumu kifo Joseph Kuria Irungu maarufu ‘Jowie’ baada ya kumkuta na hatia ya mauaji ya mfanyabiashara Monica Kimani.

Akitoa uamuzi huo mnamo Jumatano, Jaji Grace Nzioka alisema alibaini kuwa mauaji hayo ya kutisha ya Monica Kimani yalikuwa ya ‘Kusudi.’

“Hakikuwa kitendo cha kujitetea. Halikuwa tendo la kuchokozwa. Ilipangwa, ikakusudiwa na kutekelezwa.” Alihukumu Jaji Nzioka.

Jaji Nzioka amebaini kuwa hukumu aliyotoa inalingana na hatia yenyewe ya kesi na kwamba lengo lake ni kuzuia visa vya uhalifu sawia kutokea katika siku za usoni.

Alisema kuwa lengo la hukumu ni kutoa funzo na pia kumpa mhalifu fursa ya kurekebisha tabia.

Hukumu hiyo iliyosubiriwa kwa hamu imejiri baada ya muda mrefu wa vikao vya kesi hiyo pamoja na kuahirishwa kwake hivi majuzi.

Mnamo mwezi Februari Joseph ‘Jowie’ Irungu alikutwa na hatia ya kumwua Monica Kimani ambaye alipatikana ameuawa kinyama katika makazi ya Lamuria Gardens jijini Nairobi usiku wa Septemba 19 mwaka 2018.

Hukumu hiyo ilikuwa imepangwa kutolewa Ijumaa Machi 8 wiki lililopita lakini iliahirishwa kwa sababu mbalimbali ikiwemo kucheleweshwa kwa nyaraka muhimu na hata mabadiliko ya uwakilishi wa Kisheria wa Jowie.

BY MJOMBA RASHID