HabariNews

Uzinduzi wa Mombasa Press Club; Wanahabari Mombasa wausiwa Kuepuka ‘ombaomba’ Watumie Klabu Kukabili Changamoto

Huenda changamoto zinazowakumba wanahabari kaunti ya Mombasa zikapata suluhu kufuatia uzinduzi wa klabu ya Mombasa Press Club.

Uzinduzi huo uliofanyika Jumatano Machi 20, kwa ushirikiano na Baraza la wanahabari nchini MCK unajiri baada waandishi kulalamikia mazingira ya kufanyia kazi sawia na kupitia changamoto mbalimbali za kikazi, kiuchumi sawia na kupata taarifa kutoka idara mbalimbali za serikali.

Akizungumza katika uzinduzi huo Mkurugenzi wa Mafunzo na Maendeleo ya Wanahabari katika Baraza la Wanahabari nchini MCK, Victor Bwire, aliwataka waandishi kuitumia klabu hiyo kukabili changamoto zinazowakumba kupitia kuuza maudhui na kazi zao ili kujipatia kipato.

Umuhimu wa Klabu hii ni kupunguza suala la ombaomba kwa wanahabari, sisi ni wataalam masuala ya kuomba na kufuatana na watu kuitisha bahasha ni aibu. Kwa hivyo hii klabu ni njia fulani unatengeneza fedha kwa heshima na kiutalaamu zaidi kupitia kufanyia kazi maudhui yako mwenyewe kama vile habari na kuangalie vile utauza, biashara kubwa ya mwandishi wa habari ni habari.” Alisema.

Bwire aidha aliwasihi wamiliki wa vyombo vya habari Mombasa kuitumia fursa hiyo kupunguza suala la kutegemea wawekezaji na gharama za uzalishaji na badala yake kutumia klabu hiyo kununua maudhui ya habari na vipindi mbalimbali.

Akimzungumzia Gavana wa Mombasa Abdulswamad Shariff Nassir aliyehudhuria uzinduzi huo na ambaye ni mmoja wa Wamiliki wa vyombo vya habari, Bwire alisema kuwa suala la ufunguzi wa klabu za waandishi maarufu ‘Press Clubs’ limekuwa mtindo unaoendelezwa katika mataifa mengi ulimwenguni na husaidia waandishi kuendeleza taaluma yao sawia na wamiliki wa vyombo vya habari kupunguza gharama.

Na bwana Gavana wewe ni mmiliki wa sekta, press club itakusaidia kupunguza gharama za uendeshaji chombo cha habari, kwa sababu moja ya gharama kubwa ya uendeshaji ni stima na nafasi inayoathiri chumba cha habari, kwa hivyo Mombasa press club ikijipanga wanahabari wanaweza kufanya kazi kwingine na kukuuzia maudhui kwa bei mtakayoelewana na uendelee na kazi bila kujali idhaa gani anafanyia kazi.”

Ndio maana vyombo vingi vya habari duniani vimekumbatia mfumo huu kama Reuters, AFP hawana wafanyakazi wengi kama mnavyodhania kwa sababu walijua ad ana gharama za uzalishaji maudhui.”Alisema.

Kwa upande wake Gavana wa Mombasa aliyekuwa mgeni wa heshima kwenye hafla hiyo Abdulswamad Shariff Nassir aliahidi kushirikiana na wanahabari kwenye mchakato wa kutoa hamasa kwa jamii kuhusiana na maswala mbali mbali ya kimsingi.

Gavana Nasser aliahidi kutoa hamasa kwa jamii kuhusu maswala yatakayoibuka kama njia moja ya kufanikisha utendakazi wa wanahabari mjini humo akiwataka wanahabari kuchapisha taarifa zenye utu sawia na kuwa mabalozi wa kuangazia mazuri yanayofanywa na kaunti hiyo.

“Ni wazo ambalo muda wake umefika na kiini cha ujumbe ni mwafaka na mmeweka taaluma hai kila mmoja katika tasnia hii ameathirika na hali zilivyo na kuna ushindani mpya, ila hiki mlichokifanya mmeweka msingi thabiti utakaowalinda,” alisema Nassir.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali kaunti ya Mombasa wakiwemo Naibu Gavana Francis Thoya, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Ubaharia nchini KMA, Khamis Mwaguya, naye Mkurugenzi wa Kituo cha Sanaa cha Swahiliport Hub Mahmood Noor miongoni mwa viongozi wengine.

BY MJOMBA RASHID