HabariNews

Kaunti ya Kilifi yaongoza kwa visa vya Dhulma za Kihistoria za Ardhi

Kaunti ya Kilifi imetajwa kuongoza kwa visa vya dhulma za Kihistoria za ardhi ikilinganishwa na kaunti nyinginezo kote nchini zilizowasilishwa kwa Tume ya Kitaifa ya Ardhi, NLC.

Kamati ya kukusanya maoni ya wananchi walio na lalama kuhusu ardhi wanazokalia, ilieleza kwamba zaidi ya malalamishi 2,000 yamenakiliwa kutoka kaunti hiyo katika visa 3,742 vilivyonakiliwa nchini.

Akihutubia wanahabari wakati wa Kikao kinachoendela cha kukusanya maoni ya wakaazi walio na utata hapa Mombasa Mwenyekiti wa kamati hiyo James Tuitoek, alidokeza kwamba tume hiyo inakumbwa na uhaba wa fedha kutekeleza wajibu wake ipasavyo.

“Kaunti ambayo tumepokea madai mengi ni Kilifi na ile imeandikisha madai madogo ni kaunti ya Mandera ambapo iliandikisha moja pekee,shida moja tuko nayo kama tume ni uhaba wa fedha sasa tunaomba kaunti ambazo ziko karibu na Nairobi kutembelea afisi zetu.” Alisema Tuitoek

Aidha, Tuitoek alieleza kwamba wanashughulikia suala la wamiliki wasiokuwepo sawa na wananchi kulipia ardhi kwa watu binafsi ili kuona kwamba limetatuliwa akitaja hali hiyo kukithiri kaunti ya Mombasa.

“Tutafanya juhudi zote kuhakikisha madai haya yanatatuliwa tumeona Mombasa iko na wamiliki wasiokuwepo na wananchi wanalipia ardhi kwa watu binafsi.” Alisema Tuitoek

Kwa upande wao wakaazi wanaohusishwa na madai hayo waliitaka serikali kuu na ile ya kuanti kuhakikisha wanaingilia kati kuchunguza hatimiliki za wanaodaiwa kumiliki ardhi hizo.

“Tunataka serikali kuchunguza iwapo zile hatimiliki ni za kweli maanake wahusika wanahongwa kutoa hatimiliki kiholela kwa hivyo tunaomba serikali watusaidie katika jambo hili, sisi tunasema viiongozi wa kaunti lazima msimame mpitishe kauli muokoe wananchi wa Mombasa.” Walisema.

BY MEDZA MDOE