HabariNews

Waziri wa Afya Susan Nakhumicha ameonya kuwa huenda Serikali ikaamua Kuwafuta kazi madaktari wote wanaogoma.

Waziri Nakhumicha anashikilia kuwa madaktari wanakiuka agizo la Mahakama ya Leba kwa kuendelea kushiriki mgomo huo licha ya mahakama hiyo kuwaagiza wausitishe ili kutoa nafasi ya mwafaka kupatikana.

Waziri huyo alibaini kuwa madaktari hao sasa wako hatarini kupoteza kazi zao kwa kukosa kuripoti kazini na badala yake nafasi zao kuchukuliwa na madaktari wanagenzi.

“Waliagizwa na mahakama kusitisha mgomo wao; maamuzi yao yana matokeo…” alisema.

Na kuhusu Mahakama hiyo kuagiza wizara yake kutekeleza Makubaliano ya madaktari hao wanayolalamikia, Waziri Nakhumicha ametetea serikali akisema imetekeleza mkataba huo kwa ‘kadri inavyoweza.’

Hata hivyo waziri Nakhumicha alidokeza kuwa kikao kingine kati ya Serikali na madaktari kingefanyika leo baada ya kikao cha Jumatatu kugonga mwamba na kupelekea madaktari kujiondoa kwenye mazungumzo.

Haya yanajiri huku mgomo wa madaktari ulioanza Alhamisi wiki iliyopita ukiingia siku ya 8 hii leo, huku madaktari kupitia chama chao, KMPDU wakionya kuhusu kuendeleza mgomo mrefu zaidi kulingana na jinsi Serikali inavyoshughulikia matakwa yao.

BY MJOMBA RASHID