HabariMazingiraNews

Wanamazingira watilia shaka Kuafikiwa kwa Mpango wa Serikali kupanda Miti Bilioni 15 Kufikia 2030

Huku Kenya ikiungana na Ulimwengu kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Misitu, Wanamazingira kaunti ya Kilifi wametilia shaka kuafikiwa kwa azma ya serikali ya kupanda miti bilioni 15 kufikia mwaka 2030.

Haya ni kutokana na takwimu za misitu kuonekana kuwa zingali chini ambapon kwa sasa kuna asilimia 7 tu ya misitu kote nchini.

Kampeni ya kupanda miti bilioni 15 ifikapo mwaka 2030 iliyoanzishwa na serikali ili kuongeza kiwango cha misitu imetiliwa shaka ya kufanikiwa na wanamazingira kwa kile kinachotajwa kuwa takwimu za chini za misitu kufikia sasa.

Kwa mujibu wa Gabriel Itote ofisa wa shirika la Jijenge Youth Initiative kaunti ya Kilifi kwa sasa taifa la Kenya lina asilimia 7 ya misitu hali anayosema itakuwa vigumu kufikia azma ya kuongeza asilimia ya misitu na kufikia 30 ifikapo mwaka 2030.

Aliongeza kuwa kaunti ya Kilifi haijapiga hatua ya kuongeza asilimia ya misitu kutokana na changamoto ya ukataji miti kwa kiwango kikubwa kwa ajili ya uchomaji makaa.

Itote alisema mikakati ya kupanda miti pamoja na kutoa hamasa zaidi kwa wakazi kuhifadhi misitu inaendelea huku akieleza kuwa iwapo wakazi watakumbatia mpango huo asilimia ya misitu kaunti ya Kilifi itapanda na kufikia asilimia 15 katika kipindi cha kati ya miaka miwili au mitatu ijayo.

BY ERICKSON KADZEHA