HabariNews

Vijana 26 Washukiwa wa uhalifu Wakamatwa na Maafisa wa Usalama Kaunti ya Kwale

Vijana 26 wanaoaminika kuwa miongoni mwa magenge yanayowahangaisha wakaazi pamoja na wafanyabiashara mjini Diani na maeneo mengine ndani ya Kaunti ya Kwale wametiwa mbaroni.

Akithibitisha hayo Kamishna wa Kwale Stephen Orinde amedokeza kuwa vijana hao ni wenye umri Kati ya 16 hadi 26 ambao umri wao ni mdogo wala sio wa kujihusisha na visa vya utovu wa usalama.

Aidha afisa huyo alisema vijana hao watakabiliwa vilivyo na mkono wa sheria ili iwe mfano na funzo kwa wenzao wanaotishia usalama wa Kaunti hiyo.

“Juzi tumeshika washukiwa 19 Msambweni na wote wako korokoroni tupate nafasi ya kufanya uchunguzi ,umri wa vijana hao si mmoja kuna wale wa miaka 18,19 na kuendelea.” Alisema Oriende

Wakati uo huo msemaji wa serikali Mwanaisha chidzuga alibaini kuwa Serikali inachukua jukumu la kukomesha magenge hususan wale wa vipanga ambao wamekuwa wakitatiza amani na usalama.

“Kamati ya usalama wameweka mikakati kuhakikisha kwamba wanakabiliana na tatizo la usalama kaunti ya Kwale tayari kuna vijana wameshikwa wale wanaohusika na maswala ya vipanga.” Alisema Chidzuga

Itakumbukwa kwamba ni hivi majuzi tu ambapo wanafunzi wa chuo cha anuwai cha Mombasa tawi la Kwale walivamiwa na genge la vijana hao na kuwaacha na majeraha mabaya mwilini.

BY BINTI KHAMIS