HabariNews

Matembezi ya ‘Mombasa Walk Movement’ Yapania Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi

Mwenyekiti wa Vuguvugu la Mombasa Walk Movement Major Idris Abdulrahman ameeleza kuwa wanapania kuimarisha mazingira na kuhamasisha umma zaidi kuhusiana na masuala ya mabadiliko ya tabianchi wakati wa matembezi.

Katika mahojiano ya Kipekee na Sauti ya Pwani, Meja Idris amefichua kuwa vuguvugu hilo linalohusisha wanachama kutembea kwa umbali kati ya kilomita 8 hadi 10 kwa siku ili kuimarisha afya litaanzisha mpango ili kuwafaidi kiafya wanaotembea sawia na kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi.

“Kwa siku tunatembea umbali wa kati ya kilomita 8 hadi 10 hii ni afya nzuri na tunahimizana ili kukabiliana na maradhi na pia hali ya hewa sasa lazima tuwahamaishe watu na tuanze kukabiliana na uchafuzi wa mazingira.” Alisema.

Amesema matembezi hayo ambayo kwa sasa yamekuwa mtindo uliokubalika Mombasa na kaunti nyingine za Pwani sasa yatalenga zaidi kuweka mikakati bora kuhamasisha utunzaji mazingira kwa kupanda miti ili kukabiliana na hali ya hewa na mabadiliko ya tabianchi.

Matembezi yetu yamekuwa ni kama mtindo wa maisha si Mombasa pekee sasa hadi kaunti ya Kwale, Taita Taveta watu wamekubali, sasa tunakuja na mipangilio kupanda miti kukabiliana na hali ya hewa na mabadiliko ya tabianchi maana afya na hali ya hewa na mabadiliko yake inahusiana; lazima tupande miti kando kando ya barabara watu wawe na hifadhi maana kuna wale wanatembea kwa sababu mbalimbali…alisema.

Wakati uo huo aliwasihi watu kujitokeza kwa wingi kushiriki matembezi hayo ili kuboresha afya zao, vilevile akiwataka Waislamu hasa katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhan kutolegeza kamba katika suala la kuimarisha afya zao kupitia mazoezi ya aina hiyo.

BY MJOMBA RASHID