HabariNewsSiasa

LSK Yaiponda EACC Ikiitaja Kampeini ya Kukabili Ufisadi kuwa ya Unafiki

Chama cha Wanasheria nchini LSK kimekosoa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi EACC kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake kuukabili ufisadi nchini.

Rais wa LSK Faith Odhiambo ameikashifu EACC kwa kuonyesha ulegevu katika kupambana na ufisadi ambao ni donda sugu nchini.

Akizungunza jatika mahojiano na Runinga moja nchini mnamo Alhamisi Machi 28, rais huyo wa LSK alisema EACC imefeli kuukabili ufisadi kwa kushindwa kufanikisha kesi za wizi na ubadhirifu wa fedha na mali ya umma zilizowasilishwa mahakamani mara kwa mara.

Kulingana na Odhiambo kukosa kuzikabili kesi za ufisadi kutaendela kuathiri huduma za umma katika taasisi mbalimbali na kwamba huenda kukasambaratisha utoaji wa huduma hizo.

“Nahisi kuwa taasisi moja iliyowaangusha sana Wakenya ni EACC kwa sababu hata kama wanasema wataendeleza kampeini hii ya kupambana na ufisadi, je, itafikia wapi? Wanafanya nini hasa tukiona Taasisi ambayo watu walikuwa wakiogopa sana kwa kufuatilia ufisadi leo hii inaondoa kesi mbalimbali za ufisadi zilizowasilishwa mahakamani, tunatarajia nini zaidi?” alisema.

Kuhusu EACC kuanzisha kampeini ya siku 100 dhidi ya ufisadi baada ya kutoa ripoti kuhusu tatizo hilo katika taasisi za umma nchini, Odhiambo ameitaja kampeini hiyo kama unafiki akisema Tume hiyo inapaswa kuanza kampeini ya kuondoa uozo huo ndani ya tume la sivyo huenda ikashindwa kuwawajibisha watu fisadi.

Naona kampeini hii ina unafiki fulani kwa sababu nahisi Taasisi moja iliyowanagusha Wakenya kwa kweli ni hii EACC na nadhani EACC inapaswa kuanza kampeini hayo ndani ya taasisi yenyewe isafisha mifumo yake na wao wenyewe kabla kuanzisha kampeini ya kuwawajibisha Wakenya,” alisema.

Haya yanajiri siku moja tu baada ya EACC mnamo Jumatano Machi 27 kutoa ripoti ya ufisadi iliyobainisha kuwa Wizara ya Usalama ndio inayoongoza kwa visa vya ufisadi ikifuatiwa na wizara ya afya nchini.

EACC ilifichua kuwa Idara za afya za kaunti na kitengo cha Polisi wa Kawaida ndizo taasisi za umma zinazoongoza kwa ulaji rushwa.

 

BY MJOMBA RASHID