HabariLifestyleNews

Vuta Nikuvute ya Serikali na Madaktari Yazidi kulemaza Huduma za Matibabu

Wakenya wanaendelea kuhangaikia huduma za matibabu katika hospitali za umma nchini kufuatia mgomo wa madaktari unaoendelea kwa wiki ya pili sasa.

Mgomo huo ambao mnamo Alhamisi Machi 28 uliingia siku ya 14 unazidi kuendelea kuwaumiza wananchi wanaosaka huduma mbalimbali za matibabu huku madaktari wakiendelea kushikilia msimamo wao.

“Tunaomba serikali ikae chini iwaskize madaktari na waelewani maana sasa hali mbaya tunaumia…” Alisema mmoja.

“Tukifika hatupati msaada wowote na hatuna uwezo wa kuenda private,” mwengine akaongeza.

Katika kaunti ya Mombasa huduma zimeendelea kulemazwa huku madaktari kaunti hiyo wakiungana na wenzao Pwani na kote nchini kushiriki maandamano kushinikiza kutekelezwa kwa matakwa yao.

Katibu Mkuu wa KMPDU ukanda wa Pwani Dkt. Ghalib Salim amesema ni sharti Serikali itekeleze mkataba wa makubaliano yao walioafikiana tangu mwaka 2017 kabla madaktari hao kurejea kazini.

“Tumevulia kwa muda wa miaka 7 kutoka 2017 watu waliposaini ile CBA hadi sasa 2024, na katika vipengele vya CBA ke hakujatekelezwa, utamskia Gavana huyu amefanya kidogo asilimia 10 mwengine 20 mwengine 30, hakuna mtu anafikisha kutekeleza makubaliano kwa asilimia 70 ama 80,” alisema.

Mazungumzo ya pili katika muda wa wiki moja yaligonga mwamba hapo jana Jumatano baada ya madaktari chini ya muungano wao KMPDU kuondoka kwenye mkutano huo kwa kile walichokitaja kulazimishwa kurudi kazini pasi kuwepo kwa mfumo mfumo sahihi wa kurejea kazini.

Mazungumzo hayo yaliyoamrishwa na Mahakama yalishindwa kutoa suluhu, huku Serikali kudaiwa kuwalazimisha madaktari hao kusitisha mgomo wao kabla ya mazungumzo kuanza, nao madaktari wakiongozwa na Katibu Mkuu wa KMPDU Davji Atella wakiitaka serikali kukubaliana nao kuhusu mfumo wa kurudi kazini kabla ya kuamua kusitisha mgomo.

BY NEWS DESK