HabariNews

Serikali Yasitisha Uchapishaji wa Mavazi yenye Nembo za Mashirika na Taasisi za Serikali

Serikali imesitisha kwa muda uchapishaji wa mavazi na bidhaa nyingine zenye nembo ya mashirika na taasisi za serikali, kama hatua inayolenga kupunguza bajeti za matumizi.

Katika waraka, Mkuu wa utumishi wa umma Felix Kosgei ameagiza afisi hizo kuboresha utendakazi wao kwa kusawazisha matumizi yote yasiyo ya kipaumbele kulingana na miongozo iliyotolewa na hazina ya kitaifa.

Kufuatia hali hiyo ambapo ununuzi, uchapishaji na utengenezaji wa nguo za kampuni, zikiwemo t-shirt, shati, track suit na nguo zenye chapa umesitishwa.

Kosgei aidha amebainisha kwamba kutakua na usitishaji wa mara moja ununuzi wa bidhaa za matangazo kama vile kalenda, shajara, miavuli, benki za umeme, funguo, mifuko, chupa, vikombe, blanketi za kitamaduni zenye chapa (shuka) na madaftari.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa chama cha UDA Cleophas Malala alisema, chama hicho hakiko tayari kumvumilia yeyote atakayekwenda kinyume na mipango ya Serikali ya Kenya Kwanza kutimiza ajenda zake kwa wananchi.

Kulingana na Malala muda wa serikali kutekeleza ahadi zake kwa Wakenya unazidi kuyoyoma na chama hicho hakiko tayari Kwenda uchaguzini 2027 kabla ya kutekeleza ahadi zake.

Malala alibaini kuwa chama cha UDA kitafuatilia kila agizo linalotolewa na rais likiwemo la hivi punde la kuwataka wakuu wa mashirika ya serikali kuwajibikia fedha za umma.

Haya yanajiri siku moja baada ya Rais William Ruto kuagiza kwamba serikali ikiwa ni pamoja na mashirika ya Serikali kuishi kulingana na uwezo wake rais aidha akiwataka wakurugenzi wakuu kupunguza bajeti zao za matumizi ya kawaida kwa asilimia 30.

BY NEWSDESK

BY NEWS DESK