HabariNews

Rais Ruto Aagiza Mashirika ya Serikali Kupunguza Bajeti kwa Asilimia 30

Muda umeisha kwa mashirika na taasisi za kiserikali kuendelea kuandikisha hasara.

Ni kauli yake Rais William Ruto, akizungumza kwenye kikao na Wakurugenzi Wakuu wa Mashirika ya Kiserikali katika Ikulu ya Nairobi mnamo Jumanne, Machi 26.

Rais ameyataka mashirika na taasisi za serikali kupunguza bajeti yao kwa asilimia 30 na kuepuka matumizi mabaya ya fedha yakiwemo utoaji zabuni kiholela.

“Sasa kwa kuwa Uchumi umeimarika, hatuwezi kuendelea kulimbikiza deni. Kuomba mkopo kutatufikisha mahali pabaya,” alisema rais.

Ruto aliagiza maafisa wakuu hao kuwa mashirika hayo ni sharti matumizi yao yasizidi mapato yaliyokusaanywa akifichua kuwa badhi ya mashirika kwa miaka kadhaa sasa yamekuwa yakitumia fedha kupita kiasi cha kilichoratibiwa.

Na kuhusu upotevu na utumizi mbaya wa fedha katika Mashirika ya Serikali rais alisema: “Fedha ambazo baadhi ya mashirika ya umma hupata si mali ya bodi au usimamizi wao. Ni mali yaWakenya kama mapato ya uwekezaji.” Alisema.

Rais alieleza kutamaushwa na ongezeko la hali ya juu la utumizi mbaya wa raslimali za umma akisema suala hilo linahujumu utoaji mwafaka wa huduma.

Ameagiza kuwa kuanzia sasa Bajeti za Serikali na matumizi yake zitapitia ukaguzi wa kina.

“Tutapunguza matumizi kwa kuepuka kuomba mikopo kusikohitajika sana. Lazima tuwe wakweli na tufanye kile ni sahihi. Huu ndio wakati.” Aliongeza.

Alikuwa akizungumza kwenye Mkutano na Wenyeviti na Wakurugenzi Wakuu Tendaji wa Mashirika ya Serikali katika Ikulu.

BY MJOMBA RASHID