HabariNews

Mauaji Ya Shakahola; Familia Kuanza Kupokea Miili ya Wapendwa wao Iliyofukuliwa Shakahola

Serikali sasa imeanza zoezi la kupeana miili iliyofukuliwa katika makaburi ya halaiki msituni Shakahola Kaunti ya Kilifi.

Shughuli hiyo inafanyika ikiwa ni zaidi ya mwaka mmoja sasa tangu kugunduliwa kwa makaburi hayo baada ya mauaji ya halaiki kufanyika chini ya uongozi wa mshukiwa mkuu mhubiri tata Paul Makenzie na washirika wake.

Familia tatu Jumanne Machi 26 mchana zilitarajiwa kupokea jumla ya miili 7 ya wapendwa wao katika makafani ya Malindi huku familia zaidi zikiendelea kusubiri kutambuliwa kwa wapendwa wao.

Familia hizo tatu ambazo zitapokea miili ni pamoja na ile ya afisa wa GSU, Isaac Ngalla ambayo ilipoteza jumla ya watu wanane, familia ya Bella Faith Atieno pamoja na Uza Agatha wenyeji wa eneo la Magharibi mwa Kenya.

Familia ya mwisho ni ya Raphael Temba pia aliyeangamia msituni humo.

Ripoti kutoka Kwa serikali zinaonyesha kuwa zoezi hilo litaendelea hadi mwezi wa nne kabla kuelekea msituni kwa ufukuzi wa awamu ya tano.

Familia zinaombwa kufuatilia matokeo ya DNA za wapendwa wao ili waweze kupokea miili Kwa matayarisho ya mazishi.

Hata hivyo idadi kubwa ya wanafamilia wanasema hawana uwezo wa kufanya mazishi Kwa wapendwa wao wakiitaka serikali kuingilia kati na kutoa msaada sambamba na fidia Kwa familia hizo.

BY JOSEPH YERI