HabariLifestyleNews

IDD ul FITR! Serikali Yatangaza Jumatano kuwa Siku ya Mapumziko ya Kitaifa Kuadhimisha Eid

Serikali imetangaza siku ya Jumatano, Aprili 10 kuwa Siku kuu ya kitaifa ili kuadhimisha Sikukuu ya Idd ul Fitr.

Katika taarifa iliyochapishwa katika gazeti rasmi la Serikali mnamo Jumanne Aprili 9, na Waziri wa Usalama wa Ndani Prof. Kithure Kindiki, Jumatano itakuwa siku ya mapumziko ya Kitaifa ili kuwapa waumini wa dini ya Kiislamu fursa ya kuadhimisha siku kuu hiyo.

Haya yanajiri huku harakati na maandalizi ya shamrashamra za Sikukuu ya Eid ul Fitr yakinoga na kushika kasi mjini Mombasa na maeneo mengine ya taifa la Kenya, waumini wa Kiislamu wanapoelekea ukingoni mwa mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Misongamano mikubwa ya watu imeshuhudiwa katikati ya jiji la Mombasa wengi wakifurika madukani na masokoni katika mjini humo na katika miji mingine tofauti nchini kujitafutia bidhaa kwa ajili ya sherehe hizo.

Waislamu hapa nchini na kote ulimwenguni wanatarajia kuadhimisha Sikukuu hiyo ya Eid inayaoshiria kukamilika kwa ibada ya mfungo ya mwezi mtukufu wa Ramadhan, hapo kesho Jumatano au Alhamisi kwa baadhi ya waumini wanaoegemea mwandamo wa Mwezi wa kitaifa na Afrika Mashariki.

Kadhi Mkuu nchini Sheikh Abdulhalim Hussein Athman anatarajiwa kuongoza kikao cha kutangaza kuonekanwa kwa mwezi hii leo jioni kabla ya kuwatangazia mwelekeo waumini nchini.

Hata hivyo hii leo jioni waumini watatazama mwezi na iwapo utaonekana na kudhihirika nchini au eneo la Afrika Mashariki basi waumini wataswali Eid na kuadhimisha sikukuu hiyo hapo kesho na iwapo hautaonekana baadhi yao watakamilisha mfungo wa siku 30 hadi siku ya Alhamisi.

<<Sauti ya Pwani tutakuletea matangazo ya mwezi Mubashara (LIVE) kuanzia mwendo wa saa Kumi na Mbili na Nusu jioni, saa za Afrika Mashariki.>>

BY MJOMBA RASHID