HabariLifestyleNews

Rais Ruto Atangaza Kuondolewa kwa Ukaguzi wakati wa Maombi ya Vitambulisho vya Kitaifa

Rais William Ruto ametangaza kuondolewa kwa uhakiki unaofanyika wakati wa mchakato wa kutuma maombi ya Vitambulisho vya Kitaifa kwa watu wanaotoka baadhi ya makabila fulani madogo nchini.

Akizungumza wakati wa iftaar ya viongozi wa Kiislamu iliyoandaliwa Ikulu ya Nairobi, Rais Ruto amesema Serikali yake inafanyia marekebisho miongozo ya utoaji Vitambulisho vya kitaifa ili kuondoa mchakato huo alioutaja kama wa kibaguzi.

Rais amebaini kuwa kuanzia mwezi Mei mwaka huu kila mkenya atakuwa akipitia mchakato sawa wa utoaji stakabadhi zake ili kupata Kitambulisho cha Kitaifa pasi ubaguzi wa dini wala eneo analotoka.

“Kila Mkenya lazima achukuliwe sawa. Tumebadilisha sera ya zamani na tukajumuisha sera ya utoaji stakabadhi. Kuanzia mwezi Mei mwaka huu, hakutakuwa ten ana ukaguzi wa watu wanaotaka IDs (vitambulisho vya kitaifa),” Rais aliwambia viongozi wa kidini.

Amesema kila Mkenya anapaswa kuhudumiwa kwa usawa na hivyo kuondolewa kwa mfumo huo wa zamani wa uhakiki ili kufanikisha usawa kwa Wakenya wote.

Nitatoa sera ya stakabadhi kuhakikisha tuna mfumo sawia kwa Wakenya wote na tusibague kwa misingi ya dini na eneo,” alisema.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Kiislamu wakiwemo Mawaziri, Magavana, maseneta na maimamu miongoni mwa wengine.

Ikumbukwe kuwa mfumo wa uhakiki (vetting) umekuwa ukifanyika kwa miongo kadhaa sasa tangu kuanzishwa kwake mwaka wa 1990, na umekuwa ukitumika kwa watu wenye asili ya bara Asia, Waarabu na Wanubi ambao hulazimika kutoa vyeti vya kuzaliwa vya wazazi wao au mababu zao.

BY MJOMBA RASHID