Uncategorized

Jamii za Pwani Kunufaika Kiuchumi na Mradi wa Uhifadhi wa Mazingira ya Baharini

Uchumi wa jamii zinazoishi karibu na mikondo ya Bahari Hindi (Creeks) kaunti ya Kilifi na Kwale huenda ukaimarika kufuatia jamii hizo kujiunga na kushiriki mradi wa uhifadhi wa mazingira ya baharini na nchi bara maarufu COSME.

Mradi huo unaojumuisha makundi 43 ya wakazi unalenga kuwapa mafunzo ya jinsi ya kupanda na kutunza mikoko ili kunufaika kwa kiwango kikubwa.

Mradi huo wa COSME unaotarajiwa kufanyika kwa kipindi cha miaka mitatu unalenga kufanya urejesho wa miti ya mikoko katika maeneo ambayo yameshuhudia ukataji wa miti hiyo kwa wingi, kama njia ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa mradi huo Nancy Karuga, Afisa Msimamizi wa mradi huo kutoka shirika la Plan International, alisema mradi huo unapania kufanya upanzi wa urejesho wa mikoko 150,000 anayodai kuwa kupitia mafunzo watakayotoa kwa wakazi, mikoko hiyo itamea vizuri.

“Tulikuwa tukipanda mikoko kwa muda mrefu lakini ukija mwaka mwingine unapata mikoko iliharibika na kuoza, sasa tunataka kufanya kazi kwa karibu na shirika la KEMFRI na wataalamu wengine kuelelezea vikundi wakipanda mikoko vizuri wasipande kwa mikondo yam aji maana inasafisha mikoko, na mikoko inafanya vizuru kwenye mikoko halisi ili mingine kuwa rahisi kukua,” alisema.

Kwa upande wake Silas Tsuma ofisa mkuu wa shirika la uhifadhi wa misitu nchini kituo cha Sokoke, amesema tayari mabadiliko yameenza kushuhudiwa tangu jamii ilipoanza kushirikishwa kikamilifu kwenye miradi ya uhifadhi wa misitu na mazingira.

Ameeleza kuwa kwenye hafla hiyo miche 5,000 ya mikoko imepandwa huku juhudi za kuendelea kupanda miti zaidi eneo hilo lenye ukubwa wa takriban ekari 716 zikiendelea, ili kufikia azma ya kupanda miti bilioni 15 ifikapo mwaka 2032 ambayo ni asilimia 30 ya msitu.

“leo tumepanda miti 5,000, na tunaposhirikiana na mashirika tofauti tofauti kama Plan International tuna jukumu kuhakikisha tunaleta wadau mbalimbali ili kuona msitu huu unapandwa kulingana na utaratibu na utaalamu unaoleta mwelekeo mzuri.” Alisema.

Mwenyekiti wa vikundi vya uhifadhi wa mikoko maeneo ya Mtwapa, Takaungu na Kilifi Elijah Chai Chivatsi anasema kupitia hamasa mbali mbali sasa jamii imeweza kufahamu umuhimu wa uhifadhi wa miti hiyo.

“Hapo zamani upandaji wa mikoko ulikuwa na changamoto kwa sababu wengi hakuwa wakihusishwa na ndio maana haikuwa ikilindwa, kwa sasa tunashukuru shirika la Misitu KFS wamehusisha jamii mashinani na tumeshirikishwa kama jamii katika upanzi huu jamii imejua umuhimu wa kuipanda na kuilinda.” Alisema.

BY ERICKSON KADZEHA