HabariNews

Maafisa wa Upelelezi Wamnasa Mshukiwa wa Ulanguzi wa Mihadarati huko Kiembeni, Mombasa

Maafisa wa Upelelezi kutoka Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya hapa mjini Mombasa wamemkamata mshukiwa wa ulanguzi wa mihadarati huko Kisauni Kaunti ya Mombasa.

Mshukiwa huyo Zuher Ali Mohammed ametiwa mbaroni eneo la Bombo, Kiembeni akiwa na sacheti kadhaa za dawa zinazokisiwa kuwa Heroin na bangi zilizopatikana ndani ya gari lake na nyumbani mwake.

Kulingana na taarifa iliyochapishwa katika mtandao wa X wa DCI Kenya inaarifiwa mshukiwa huyo amenaswa mapema Jumatano Aprili 17, katika oparesheni iliyofanywa na maafisa kufuatia kudokezewa taarifa na wananchi.

Aidha mshukiwa huyo amenaswa na pesa taslim shilingi elfu 26,250 na Dola 200 za Kimarekani, mizani ya kupimia uzito, bahasha za kufungia bidhaa na simu tatu za rununu zinazoaminika kuwa taarifa za washirika wake.

Vile vile maafisa hao wamelinasa gari lake linaloaminika kutumika kuendeleza uhalifu huo.

Mshukiwa huyo anatarajiwa kufikishwa Mahakamani Mombasa hapo Alhamisi Aprili 18 kufunguliwa na kujibu mashtaka.

BY MJOMBA RASHID