HabariNews

Wanahabari wa Pwani wapata Mafunzo ya Mabadiliko ya Tabianchi, Wausiwa Kuangazia taarifa za Kukabiliana na Athari zake mapema

Serikali imeahidi kushirikiana na waandishi wa habari eneo la Pwani na kote nchini kwa jumla kuangazia maswala ya mabadiliko ya Tabianchi.

Akiongea katika warsha ya mafunzo kwa wanahabari jinsi ya kuangazia maswala ya Mabadiliko ya Tabianchi iliyoandaliwa na Baraza la Wahariri nchini KEG Msemaji wa Serikali nchini Dr. Isaac Mwaura alikiri kuweko kwa pengo kati ya wanahabari na maafisa wa Serikali hali iliyopelekea ugumu wa kikazi wakati wa kuangazia matukio na taarifa.

Alisema ofisi yake ikishirikiana na Wizara ya Mazingira itakuwa mstari wa mbele kuhakikisha ushirikiano mwema kati ya Muungano wa Wahariri (KEG) kwa kuwawezesha waandishi kupata elimu ya mabadiliko ya Tabianchi.

“Sasa basi naahidi kujitolea kwa Afisi yangu, itakuwa sehemu ya mpango wa ushirikiano wa mafunzo ya wanahabari ya Mabadiliko ya Tabianchi kati ya Wizara ya Mazingira, Shirika la maendeleo la Ujerumani, GIZ na Baraza la Wahariri KEG.”

Mwaura akisema anatarajia kufanya kazi na waandishi kote nchini kupitia vilabu vyao ili kuweka uhusiano mwema kati ya serikali na waandishi wa habari.

“Tungependa kujiunga nanyi ili pale mnapofanya mafunzo haya ya wanahabari kaunti mbalimbali nchini tunaweza kupanga na kuleta uhusiano mwafaka wa Serikali na afisi ya mawasiliano, na kwa baraza la Wahariri nawapongeza na naunga mkono moja kwa moja nikitazamia kufanya kazi hasa na waandishi kupitia Vilabu vya wanahabari kote nchini.” Alisema Mwaura.

Martin Masai mmoja wa Muamana (trustee) wa Baraza la Wahariri nchini (KEG) alisema Kama baraza wapo tayari kushirikiana na kufanya kazi  na kila sekta na idara mbalimbali serikali kufanikisha lengo la kuifahamisha jamii.

Msemaji wa Serikali Dr. Isaac Mwaura akishauriana na Martin Masai, Mdau wa Baraza la Wahariri, KEG

Alisema lengo la vyombo vya habari ni kuelimisha na hivyo licha ya kutaka uwazi na ushirikiano kutoka serikalini wanahabari pia wanapaswa kuwa wazi na kuangazia masuala jinsi yalivyo kwa taarifa sahihi kutoka kwa idara husika.

“KEG imejitolea kufikia kila shirika itakayofanikisha kazi zetu na kuturahisishia. Tukitaka serikali iwe wazi na ijitolee kutoa taarifa hitajika, pia sisi tunahitajika upande wetu waandishi kuwa wazi na tunataka Wakenya waelewe jinsi tunavyofanya kazi.Alisema Bw. Masai.

Kwa upande wake Afisa Mwakilishi wa Mawasiliano katika Wizara ya Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi Temesi Mukami alisema warsha hiyo ilikuwa ya kufana hasa katika kubaini changamoto pamoja na mapendekezo ambayo yatasaidia pakubwa waandishi katika kuandika na kuripoti maswala ya mabadiliko ya tabia nchi.

Temesi akisema watabuni mtaala maalum ambao utatumika na taasisi mbalimbali za mafunzo pamoja na waandishi katika maswala ya mabadiliko ya tabia nchi.

Kutokana na mafunzo haya tutaunda mtaala utakaowakilisha sehemu muhimu katika tasnia ya habari ya Kenya katika masuala ya kuangazia taraifa za mabadiliko ya tabianchi. Kasha tutakuwa na mchakato wa kuuidhinisha mtaala huo ambapo tutaleta wataalamu wakiwemo Wahariri na ikiwa tayari tunaufanyia kazi.

Mtaala huu utasalia kuwa stakabadhi muhimu ya mwelekeo inayotoa maelekezo kwa wanahabari na tutaujumuisha katika mtaala wa mafunzo ya taasisi za Kenya. Alisema.

Mwanasayansi Mtafiti wa masuala ya Tabianchi Dr. John Recha aliyekuwa miongoni mwa wadau na mmoja wa mtoaji mafunzo kwa waandishi wa habari alieleza athari za mabadiliko ya tabianchi katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya kilimo, uchumi, kawi, afya na maji, huku akiwalaumu wanahabari kwa kutoangazia kwa kina masuala hayo.

Suala moja tumechunguza na kubaina kama timu ya wanasayansi kwa muda wa miaka 10 hadi 20 iliyopita ni kuwa athari ya mabadiliko ya tabianchi zimekuwa kubwa, ikiathiri sekta mbalimbali katika jamii, na kiwango cha kuangazia taarifa hizi kile kinachopelekea athari hizi imekuwa haba sana.Alisema.

Dkt. Recha alisisitiza kuwa kiwango cha wanahabari kuangazia taarifa za mafuriko yanayoendelea kushuhudiwa nchini ambapo walishindwa suala la athari kwa kutoa taarifa ambazo zingeweza kukabili majanga kwa wakati kuliko kusubiria majanga kutokea na kuyaripoti.

Ni kauli iliyoungwa mkono na Hamisa Zaja Afisa na mshikadau wa shirika la Maji na Ufanisi, aliyewataka wanahabari kuwa mstari wa mbele kuangazia jinsi wananchi wanavyoweza kupata taarifa za suluhu la mabadiliko ya tabianchi na kutumia fursa zilizopo.

Bi. Hamisa Zaja akihutubia wanahabari

“Ni vyema wananchi wakapata kuangaziwa taarifa za mapema za jinsi ya kuepukana na athari zozote kabla ya kujiri, na sasa hivi kuna mafuriko muhimu wakipata taarifa zaidi ya suluhu na kuweza kutumia fursa hizi kwa manufaa ya baadaye.” Alisema Bi. Zaja.

Katika warsha hiyo ya mafunzo ya siku mbili iliyoanza Aprili 29 hadi 30 mjini Mombasa, zaidi ya wanahabari 30 wakiwemo wahariri, watangazaji na waandishi wa habari walinufaika na mafunzo ya kuangazia mabadiliko ya Tabianchi, chini ya usimamizi wa Baraza la Wahariri (KEG) na Shirika la Maendeleo la Ujerumani, GIZ.

BY RASHID (MJOMBA) R. ALI