HabariNews

Ruto Akashifu Shambulizi Lililosababisha Kifo Cha Hakimu Monica Kivuti

Rais William Ruto amekashifu shambulizi lililosababisha kifo cha Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Makadara Monica Kivuti.

 Alielezea kifo chake kama “kisichokubalika” na kitu ambacho hakipaswi kutokea tena.

 “Makabiliano, vitisho, au mashambulizi ya aina yoyote dhidi ya maafisa wa mahakama hayakubaliki, ni ya uhalifu, na ni dharau kwa utawala wa sheria,” alisema.

 Aliwahakikishia usalama wao wanapotekeleza majukumu yao.

Kiongozi wa Nchi alikariri kuwa polisi wapo ili kuhakikisha usalama wa kutegemewa kwa Wakenya.

Aliwataka polisi kuendelea kuwa waaminifu kwa kiapo chao cha utumishi.

 “Kwa hali yoyote wasiache wajibu huu muhimu au kugeuka kutoka kwa jukumu lao la ulinzi na kuwa vitisho kwa usalama wa watu,” aliongeza.

 

 Akitoa rambirambi zake, Rais Ruto alisema nchi imempoteza mtaalamu shupavu na mchapakazi wa mahakama ambaye alihudumia Wakenya kwa kujitolea.

“Mwenyezi Mungu awape nguvu ya kustahimili msiba huu.”

BY CYNTHIA  OCHIENG