HabariNews

Masomo Yavurugwa kwa Muda Polisi Wakirusha Vitoza Machozi Kutawanya Waandamanaji

Shughuli za masomo zilitatizika kwa muda mnamo Jumatano Juni 19, katika shule ya Upili ya Wasichana ya Coast Girls mjini Mombasa baada ya polisi kurusha vitoza machozi kuwatawanya waandamanaji.

Inaarifa kuwa mamia ya waandamanaji walikuwa wamekita kambi katika kituo cha Polisi cha Central kutoa malamishi yao ya kupinga mswada tata wa fedha wa 2024.

Polisi wamelazimika kurusha vitoza machozi kuwatawanya, ambapo moja ya vitoza machozi hivyo kimepenyeza na kufika ndani ya shule hiyo inayopakana na kituo hicho cha polisi.

Katika ukanda wa Video ulioonekana na Sauti ya Pwani FM na unaoendelea kusambaa mitandaoni umeonesha wanafunzi wakitoka madarasani mwao wakikimbilia sehemu salama kupata hewa safi.

Polisi wamekuwa na wakati mgumu hasa baada ya kutaka kuwazuia wasiandamane Katikati ya mji wa Mombasa kwa madai kuwa hawakuwa na kibali rasmi lakini baadaye wakaruhusiwa baada ya kupata idhini.

Waandamanaji hao wengi wakiwa vijana wa kizazi kipya maarufu Gen Z wameendelea na maandamano yao pasi kujali mvua iliyokuwa ikinyesha huku wakiwa wamebeba mabango yenye jumbe za kupinga ushuru dhalimu na mswada tata wa fedha 2024.

BY MJOMBA RASHID