AfyaFoodHabariLifestyleMakalaMazingiraNews

WAKULIMA WANAWAKE WAFAIDIKA VILIVYO KWA KUKUMBATIA TEKNOLOJIA KWENYE UKULIMA.

Maisha ya wakulima wanawake wadogo wadogo wadi ya Junju eneo bunge la Kilifi kusini yanazidi kuimarika kufuatia wakulima hao zaidi ya 500 kukumbatia mbinu mpya za teknolijia ya ufugaji wa kuku na upanzi wa mimea.

Kufuatia mafanikio hayo, sasa wakulima hao wanapanga kuandaa maonesho ya kilimo mwezi Oktoba ili kushinikiza watu wengi  zaidi kushiriki kilimo.

Kundi hilo linalojumuisha wajane na wanawake wanaopitia hali ngumu za uchumi limeonekana kuwa njia ya kukwamuwa jamii eneo hili kutoka kwa lindi la umasikini kwa kuwafunza mbinu tofauti tofauti za kilimo biashara.

Kulingana na Crispus Mwaganda Saidi mwenyekiti kundi la wakulima la MATENDO CBO, wanaendelea kuwafunza wakulima jinsi ya kutumia teknolojia ya kisasa katika kuendeleza shughuli hizo za ukulima ili kuongeza faida.

Ameeleza kuwa kwa sasa wanauwezo wa kupata vifaranga zaidi ya 300 kila baada ya siku 21 kufuatia kupata mashini ya kusaidia kuanguliwa kwa vifaranga, akiongeza kuwa kwa kutumia teknolojia wameweza kuepusha kusambaa kwa magonjwa ya kuku.

“Katika hii teknolojia ya kutumia hii mashini ya kusaidia kuangua vifaranga inatuwezesha kupata vifaranga 300 kwa kila baada ya siku 21hivyo tunaona uzalishaji wa kuku unaongezeka na hiyo ni hatua ya kwanza.

“Katika hatua ya pili uhifadhi wa kuku kupitia teknolojia hii mpya unapunguza changamoto ya kusambaa kwa magaonjwa ya kuku na vile vile utunzaji wa kuku unakuwa wa hali ya juu.”  alisema Mwaganda.

Kwa upande wao wakulima hao wakiongozwa na Claris Nazi Mwangala na Mary Maitha wanasema kupitia kushiriki kilimo wanaendelea kujiimarisha kimaisha na hata kulipa karo za shule za watoto wao.

Aidha wametoa wito kwa wanawake ambao hawana njia ya kupata pesa kushiriki kilimo ili waweze kujikimu kimaisha pamoja na kusaidia familia zao.

“Nashukuru kwa kuwa napata mafunzo mazuri kuhusu ukulima na ufugaji wa kuku ili kutuinua sisi wanawake ambao tuko chini ili tukaweze kujiendeleza wenyewe.” alisema Nazi.

“Naona faida nyingi sana, kina mama wamechangamka sana manake ukiwa nyumbani peke yako huwezi kujifunza chochote lakini ukiungana na wenzako  unapata mafunzo mengi kwa mfano mimi, inanisaidia sana kwa upande wa kulipa karo za shule baada ya kuuza bidhaa zangu.” alisema Maitha.

 

ERICKSON KADZEHA.