HabariMombasaNews

Maswali Yaibuka Wizara ya Madini na Uchumi wa Baharini Kutumia Shilingi Bilioni 1.6 Kuhesabu Samaki

Wizara ya Madini na Masuala ya Uchumi wa Baharini ilitumia shilingi Bilioni 1.6 kukagua idadi ya samaki katika Bahari Hindi.

Imebainika kuwa katika mwaka wa Kifedha 2023/2024 Wizara hiyo ilipewa fedha hizo kufanya ukaguzi huo, hali iliyozua tumbojoto na maswali mengi kutoka kwa wabunge.

Katika kikao cha Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Uchumi Samawati na Unyunyuziaji Maji, Waziri Hassan Joho na Katibu wa Wizara hiyo Muthoni Njagi wametakiwa kueleza iwapo nchi ilipokea thamani ya fedha zilizotumika katika zoezi hilo.

Katika kujibu hilo, timu ya Waziri Joho imeeleza kuwa Ukaguzi wa kiwango cha samaki ni zoezi la kilimwengu linalofanyika katika mataifa ambayo yana nia kuu ya kuwekeza katika masuala ya uchumi wa baharini.

Joho ameongeza kuwa tathmini na ukaguzi wa hali na kiwango cha samaki Bahari Hindi ni muhimu sana hasa kwa taifa la Kenya linaposaka wawekezaji kuleta meli zao za uvuvi nchini.

Hata hivyo wabunge wameonekana kughadhabishwa baada ya timu ya Joho kuomba nyongeza ya shilingi 600 milioni ili kukamilisha awamu ya kwanza ya zoezi hilo, wabunge wakihoji kwa nini timu hiyo ilihitaji fedha zaidi ikiwa tayari tathmini ilifanywa.

Ikumbukwe kuwa Tathmini ya Kiwango cha samaki (Fish stock assessment) ni mchakato wa kukusanya, kuchambua, na kutoa taarifa ya hali ya samaki na maeneo ya kuzaliana ili kukadiria wingi na kiwango cha uzalishaji.

By Mjomba Rashid